Wafuasi wa chama tawala cha ANC wametoa wito kwa meya wa jiji la Johannesburg aliyemkashfu Rais Cyril Ramaphosa kwenye Facebook kwa kumwita “msaliti anayenuka” achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuchochea mgawanyiko.
"ANC inalaani kwa nguvu zake zote matusi yanayomlenga mtu wa aina ya rais, komredi Cyril Ramaphosa, ambayo yanatolewa na viongozi wa ANC na wanachama wengine katika mitandao ya kijamii," msemaji wa chama, Pule Mabe alisema katika taarifa yake.
Kauli hiyo ya chama imekuja baada ya ripoti kuandikwa katika gazeti la The Citizen kwamba meya wa Manispaa ya Dihlabeng katika jimbo la Free State, Lindiwe Kambule Makhalema alimwita Ramaphosa kuwa ni "msaliti" katika kundi maalum la Facebook.
Makhalema alikuwa akijibu swali lililoulizwa na mwanachama mwingine katika kundi hilo.
Ni watumiaji wa Facebook tu tena waliohakikiwa na wanachama watiifu kwa ANC ndio pekee wanakubaliwa kwenye kundi hilo.
Gazeti liliripoti kwamba mwanachama mmoja kwenye kundi hilo aliwauliza swali wenzake wamtajie "msaliti mkubwa anayenuka" ambaye wao walikuwa wanamjua na Makhamela alijibu "Ramaphosa". Mwanamama Lindiwe hakuwa tayari kuomba msamaha alipoulizwa juu ya majibu hayo.
Mabe alisema wameziagiza kamati tendaji za majimbo ya Free State na Gauteng kukutana na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya meya kwa “kumkashfu hadharani" Ramaphosa.
Mchakato wa kinidhamu utakuwa wa kwanza chini ya sera yake ya mtandao wa kijamii.