UMENASWA! Ndivyo unavyoweza kusema kwani kila mtu alikuwa na hamu ya kuuona mjengo unaodaiwa kusababisha ugomvi kati ya familia ya Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Hamisa Mobeto.
Baada ya wenye ubuyu wao hivi karibuni kueneza taarifa kwamba mama wa mwanamuziki huyo, Sanura Kasim ‘Bi Sandra’ na wanafamilia wengine wanaomuunga mkono wamenunia kile kinachohisiwa kuwa Diamond amempangia Mobeto mjengo wa gharama, ambapo OFM juzikati waliamua kuufungia kazi na kuusaka.
Sakasaka kila kona ya Jiji la Dar, mara paaa; timu ya wanasa vya mafichoni ya Amani ilitinga eneo la Bahari Beach, Tegeta ambako inadaiwa mwanadada huyo mwenye fani ya mitindo nchini amepangishiwa nyumba ya ghorofa na mzazi mwenzake ikimaanishwa Diamond.
KWA NINI WAMENUNA?
Sosi alidai kuwa familia ya Diamond hasa mama yake hawapendi wanawake wanaopenda kitumia ‘kitonga’ kwa kumchuna pesa mwanamuziki huyo.
“Zari hatoki midomoni mwao kwa kuwa ni mwanamke anayejiweza, lakini hawa wenzangu na mimi akina Mobeto hata kama wanatumia fedha zao kufanya vitu, familia inajua wamepewa na Diamond.
“Ndicho kilichomponza Mobeto, hizi chokochoko nyingine zote ni za nyongeza tu, lakini nyumba hiyo ndiyo mchawi mwenyewe,” sosi alidai.
OFM KAZINI TEGETA
Kuna maeneo hapa Dar ukiyaingia inabidi kichwa kinase vizuri netiweki vinginevyo unaweza kugeuka kioja watu wakakucheka, walipoibukia OFM hapo Bahari Beach si pa kitoto, ilikuwa ni kujiuliza; “ni ipi sasa kati ya hizi?”
Baada ya ukaguzi ulioenda shule wa OFM, kikosi kazi makini kilibaini kuwa moja kati ya majumba mazuri yaliyokuwa mbele yao ni mjengo anaoishi Mobeto, macho yalikula nakshi si za kitoto kwenye nyumba hiyo.
Mjengo huo ni balaa, kwanza mtaa wenyewe ni uzunguni hasa maana hauna kelele na nyumba zote zilizopo eneo hilo ni za hadhi ya wenye nazo, angalia hata picha ukurasa wa mbele unadhani kwa akina Kayumba utaziona nyumba kama hizo?
Hata hivyo, wazee wa kazi zao walifika hadi kwenye geti la nyumba hiyo inayodaiwa anaishi Mobeto kisha kugonga geti lakini wenyeji hawakuitikia.
Ndani ya mjengo huo zilisikika sauti za watu zikiongea, hapo ndipo OFM ilipoingia shaka kidogo kwamba huenda si kwa Mobeto, maana ni vipi asiitikie hodi za wageni, anaringia kitu gani?
UAMUZI WA KUHAKIKISHA
Kwa wachunguzi wetu suala la kubahatisha halitakiwi kupewa nafasi, baada ya wasiwasi ambao siku zote ndiyo akili kuibuka ikabidi makamanda washauriane kufanya uhakiki wa anayeishi kwenye nyumba hiyo.
Mtu wa kwanza kufika katika akili za mmoja wa makamanda wa OFM alikuwa ni Balozi wa Shina Namba 6, aitwaye Claud Andrew Kayako wa Mtaa huo anaoishi Mobeto kwamba angetegua haraka kitendawili cha uhakika uliohitajika.
MSIKIE BALOZI
Balozi huyo alieleza kuwa anao uhakika kuwa Hamisa anaishi mtaani pale na kuonesha jengo husika (Picha ukurasa wa mbele) na kwamba anaishi na ndugu zake.
“Kweli alihamia hapa ila tarehe siikumbuki, ni siku za hivi karibuni.
“Yupo hapa na anaishi yeye pamoja na mama yake na watoto zake wawili, na ndugu yake mwingine anaitwa Mwajuma na mwingine wa kiume lakini simjui jina.
“Mama yake na ndugu zake huwa wanatusalimia kutujulia hali, na yeye huwa tunamuona akitoka na gari la rangi ya bluu bahari na kwenda kwenye shughuli zake. Mama yake huwa anatoka na gari nyeupe,’’alisema Claud akiziacha kwatu roho za makamanda wa OFM.”
HADHI YA NYUMBA
Kama ilivyoelezwa, mjengo anaoishi Mobeto si wa kitoto, kwa muonekano wa macho tu lakini hata hadhi yake ukiutazama unaupa thamani ya mamilioni.
“Ni nyumba ya gharama sana, hata kodi yake inaweza kufikia milioni 3 kwa mwezi, maana ile pale (anaonesha nyumba nyingine jirani) rafiki yangu amepanga kila mwezi analipa milioni mbili na nusu, ndani kaweka hadi ofisi,” kijana mmoja anayeishi eneo hilo ambaye hakutaka kutaja jina aliliambia Amani kujaribu kusaidia ukadiriaji wa kodi ya pango.
MOBETO NA KODI YA MIL. 3?
Hivi huyu dada huwa anafanya kazi gani zaidi ya huo uanamitindo wake?
Ina maana ana hela za kuweza kupanga nyumba ya milioni 3 kwa mwezi kwa usawa huu?
Kama anahongwa ndiyo ahongwe milioni 3 za nyumba tu; hizo ni mbali na za mavazi, chakula, mapambo na mambo mengine, ama kweli huyo anayemhonga atakuwa na ‘mihela’.
UNAJIULIZA PAMOJA NASI
Kama ambavyo ulikuwa ukisisimka ulipokuwa ukisoma viulizo hapo juu, wengi katika mijadala wamekuwa wakiuliza ughali wa maisha ya mastaa wa kike Bongo ukilinganishwa na kipato chao na si kwa Mobeto tu.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na Amani mara kadhaa umekuwa ukibaini kuwa, kazi za wazi wanazozifanya mastaa wa kike hapa Bongo ni muziki, uigizaji, uanamitindo na sanaa nyingine ambazo kwa namna moja ama nyingine haziwawezeshi kuishi maisha ya anasa.
Pengine maswali ya wengi katika maisha ya mastaa wetu ni ‘wapi wanapata hizo fedha za ziada’, wapo watu wamekuwa wakiwahukumu kuwa huenda wanafanya biashara ya ukahaba, jambo ambalo Amani haliwezi kuliamini hata kama itakuwa kweli kwa sababu haijapata hoja za kuweka mkononi.
NI LAZIMA MOBETO APANGISHIWE?
Pamoja na kwamba Mobeto amekuwa mgumu kupokea simu lakini bado haiwezi kuwa sawa kumtuhumu kuwa amepangishiwa nyumba na Diamond kwa sababu hana ulazima.
Inawezekana katika kipato na jasho lake anaweza kuwa na huo uwezo wa kufanya ‘fujo mjini’ ili kufurahia maisha na familia yake kama waswahili wasemavyo; ukipata tumia, ukikosa jutia.
Maana ubuyu mwingine uliopo mjini ni kwamba mwanamitindo huyo anamiliki duka kubwa la nguo maeneo ya Kijitonyama, duka ambalo nalo wambeya wa mjini wamekuwa wakisema amefunguliwa na Diamond bila kuweka ushahidi mezani.
PICHA BADO LINAENDELEA
Picha la familia ya Diamond na Mobeto bado linaendelea mpaka hapo kitakapoeleweka kati ya Zari na Mobeto atakayekuwa mkwe halali wa familia hiyo kwani pande bado zinavutana, wapo wanaomtaka Zari lakini wapo wanaomtaka Mobeto.
NENO LA MHARIRI
Gazeti hili linamsihi Diamond kuangalia furaha yake kwani mwisho wa yote yeye ndiye atakayeingia kwenye ndoa na kuishi maisha ya kindoa, ausikilize moyo wake, iwapo utaangukia kwa Hamisa basi heri lakini kama moyo utaangukia kwa Zari nayo ni heri kwani wote ni wazazi wenzake au ikiwezekana afunge nao ndoa wote wawili kwani dini yake inamruhusu.