Takriban watu 15 wamefariki katika moto mkubwa uliokumba soko moja katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.
Zaidi ya watu 50 walijeruhiwa katika moto huo uliotokea katikati ya usiku na kusababisha uhuribifu wa mali nyingi.
Soko hilo la Gikomba ndio soko kubwa zaidi katika mji huo na moto hutokea mara kwa mara swala linalosababisha uvumi kwamba huenda kuna watu wanaochoma soko hilo, kulingana na gazeti la The Standard nchini Kenya
Huduma ya ambalensi ya St John inasema kuwa moto huo ulianza saa nane za usiku Alhamisi afajiri kabla ya kuenea katika nyumba zilizopo karibu na vibanda vya soko hilo kabla ya kudhibitiwa baada ya dakika 90.
Baadhi ya waathiriwa walichomwa huku wengine wakivuta moshi wenye sumu walipojaribu kuokoa mali yao.
Maafisa wa hospitalini wanasema kulikuwa na watoto watano miongoni mwa waliofariki.