John Kelly ambaye ni msaidizi wa karibu wa rais Donald Trump ameripotiwa kusema kwamba ikulu ya White House ni mahali duni pa kufanyia kazi akitaja mizozo ya kila mara kwenye ikulu hiyo na uvujaji wa siri kama baadhi ya changamoto ambazo ameshindwa kutatua.
Matamshi ya Kelly ambayo yalichapishwa na jarida la New York Times hapo jana ni mojawapo ya visa vya uvujaji kutoka ikulu ya White House ambavyo vinaashiria kudodora kwa mazingira ya kazi katika ikulu hiyo chini ya utawala wa Trump. “Wengi wanaofanya kazi White House wanaonyesha dalili ya kutaka kujiuzulu au kutokuwa na haja,” jarida hilo lilisema.
Kelly ambaye alistaafu kama jenerali katika jeshi aliteuliwa na Trump kuwa mkuu wa utumishi wa umma mwaka jana.
Wakati wa kuteuliwa kwake Kelly alikwa na ushawishi mkubwa kwa Trump kabla ya ushawishi huo kuisha. Mapema huu mwaka Kelly aliripotiwa kuonyesha kukerwa na hali ya kazi na kutishia kujiuzulu.