Mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Babati mkoani Manyara, alikamatwa Oktoba 15, mwaka 2017 katika mji mdogo wa Himo nje kidogo ya Manispaa ya Moshi akiwa na kilogramu 10 za dawa za kulevya aina ya mirungi.
Mary ambaye anaendelea kusota mahabusu, alijifungua mapacha hao ambao ni Norin na Nora, Aprili 8, mwaka huu katika Hospitali ya Rufani ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi.
Hakimu Meena, alijikuta akitoa pongezi hizo, muda mfupi baada ya mshtakiwa huyo kupanda kizimbani kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi inayomkabili ya kusafirisha dawa za kulevya.
Awali, wakati mahakama hiyo inaanza usikilizaji wa kesi hiyo, mwendesha mashtaka wa serikali, Lilian Kowero alidai kwamba kesi hiyo namba 182 ya mwaka 2017, ilikuja kwa ajili ya kutajwa.
“Mheshimiwa, kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa kwa sababu upelelezi wake bado haujakamilika, kwa hiyo tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa,”alidai Kowero.
Baada ya maelezo hayo ya mwendesha mashtaka huyo, Hakimu Meena alikubaliana na ombi hilo ambapo kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Juni 27, mwaka huu.
Aidha, mahakama hiyo imeeleza kwamba dhamana ya mshtakiwa huyo ipo wazi na anachotakiwa kukifanya ni kuwa na wadhamini wawili ambao ni wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro, ambao watalazimika kusaini bondi ya Sh. 500,000 kila mmoja kama dhamana.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Oktoba 24 mwaka jana akikabiliwa na kesi ya usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi.