Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Taifa Chama cha Wananchi CUF, Julius Mtatiro amewapongeza viongozi wa Chama chake wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama Maalimu Seif kuweza kukamata fedha ambazo zingemfukuzisha Uanachama Katibu huyo.
Mtatiro ameyasema hayo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff akishirikiana na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara Mhe. Joran bashange na Wakurugenzi wa Kitaifa kufanikiwa kuzuia kutoka Tsh Milioni 600 zilizoingizwa kwenye akaunti ya Prof Lipumba na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Mtatiro amesema kuwa Msajili wa Vyama ameidhinisha na kupeleka TZS Milioni 600 kwenye akaunti ya Lipumba na genge lake, bila kujali kuwa Mahakama Kuu imemkataza hadi pale Mashauri yaliyoko Mahakamani yatakapokamilika.
Akifafanua suala hilo Mtatiro amesema Fedha hizo zilipangwa kutumika kuitisha Mkutano Mkuu feki ambao ungelimfukuza uanachama Katibu Mkuu kwa Baraka za Serikali na Msajili Mutungi ili sasa CUF igeuzwe kuwa tawi la CCM.
Hata hivyo Mtatiro amesema kuwa pamoja na kuwa Mutungi amekeaidi agizo la mahakama, Lipumba na watu wake wameishia kuziona fedha kwenye akaunti lakini hawatazitoa maana benki imetii amri ya Mahakama.
Mapema leo akizungumza na East Africa Breakfast Kaimu katibu mkuu wa CUF upande wa Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya amemshukia Maalim Seif na kudai alikuwa na lengo la kukiua chama hicho, ndio maana aliweza kuzuia chama kisipate ruzuku kwa nchi nzima baada ya mgogoro wa mwaka 2016.
Sakaya amesema chama hicho kimepitia katika wakati mgumu ambapo fedha zote zilizuiliwa na Maalim Seif kwa kuandika barua kwenda kwenye taasisi zote za kifedha pamoja na serikali kuzuia wasiendelee kutoa ruzuku kwa chama hicho.
Mahakama Kuu ya Tanzania ya ilimzuia Msajili wa Vyama vya Siasa, Hazina ya Nchi, Wizara ya Fedha, Mabenki yote kutotoa fedha za Chama cha Wananchi CUF na kumpatia Lipumba.