JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, limewakamata watu wanaodhaniwa kumuua kwa kumnyoga kwa kumvunja shingo mtoto wa jamii ya kifugaji aliyetambulika kwa jina la Chanya Rugwashi (12).
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Jemen Mushi, alisema baada ya watu hao kutekeleza unyama huo, waliiba kondoo wawili na kuwachinja na kuondoka na nyama.
Kamanda Mushi alisema tukio hilo lilitokea Juni 20 katika eneo la mto Nampungu katika Kitongoji cha Matikiti Mashambani katika Kijiji cha Nambalapi.
Kamanda Mushi alifafanua kuwa marehemu Rugwashi alikutwa akichunga mifungo mingi wakiwamo ng'ombe, mbuzi na kondoo, lakini watu hao baada ya kufanya mauaji hayo waliiba kondoo wawili tu.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Mushi amewaomba wananchi ambao wanawafahamu watu waliotekeleza unyama huo kulisaidia Jeshi la Polisi ili kuwakamata haraka na kupisha vyombo vya sheria kutekeleza wajibu wake.
Kaka wa marehemu Rugwashi, Bundala Rugwashi, alisema kuwa mdogo wake alipotea Juni 20 na kwamba baada ya kubaini hali hiyo, walianzisha msako katika msitu huo na kufanikiwa kuupata mwili wake Jumamosi ukiwa umening'inizwa katika mti.
Alisema baada ya tukio hilo walitoa taarifa kwa viongozi wa serikali ya Kata ya Masonya na baadae kituo cha polisi.
Taarifa ya uchunguzi wa mwili wa marehemu Rugwashi iliyotolewa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Dk. Vitaris Lusasi, inaeleza kuwa chanzo cha kifo hicho ni kuvunjika shingo.