Mwanaanga maarufu kutoka Marekani Buzz Aldrin amewashtaki watoto wake wawili na meneja wa zamani wa biashara zake akidai kwamba waliiba pesa zake.
Aidha, anadai walimharibia sifa ambazo amejizolea katika maisha yake.
Kesi hiyo, ambayo ilifichuliwa Jumatatu, iliwasilishwa katika mahakama moja mjini Florida wiki moja baada ya watoto wake kuwasilisha ombi mahakamani wakitaka waruhusiwe kuchukua udhibiti wa fedha zake.
Jamaa zake walikuwa wamemwambia jaji kwamba anahitaji mlezi wa kumwakilisha kisheria kwa sababu uwezo wake wa "kufikiria umeshuka sana".
Katika mahojiano na gazeti la Wall Street Journal wiki iliyopita, Aldrin ambaye ni kanali mstaafu wa jeshi la wanahewa la Marekani alisema: "Hakuna mtu atakayekaribia kufikiria kwamba ninaweza kuwekwa chini ya mlezi."
Kwenye kesi hiyo, anadai kwmaba mwanawe wa kiume, na binti yake pamoja na meneja wake wa zamani Christina Korp pia walivuruga uhusiano wake wa kimapenzi na watu wengine na kumzuia kuoa tena.
Mzozo unahusu zaidi usimamizi wa kampuni yake ya kibinafsi, Buzz Aldrin Enterprises, na shirika la hisani kwa jina ShareSpace Foundation.
Katika ombi waliloliwasilisha mahakamani, wanawe Andrew Aldrin, 60, na Janice Aldrin, 60, walisema baba yao hivi karibuni ameanza kujihusisha na marafiki wapya ambao wanajaribu kumpotosha na kumtenganisha na familia yake.