Museveni Awawekea Ulinzi Wabunge

Museveni Awawekea Ulinzi Wabunge
 Katika juhudi za kukabiliana na wimbi la hivi karibuni la mauaji ya watu mashuhuri, wabunge wataanza kulindwa na askari wa Jeshi la Ulinzi wa Watu wa Uganda (UPDF), imefahamika.
Uamuzi huo ni matokeo ya makubaliano yaliyofikiwa Jumanne katika mkutano wa ndani kati ya wabunge na Rais Yoweri Museveni.
Katika mkutano huo, wabunge wakionekana kushtushwa na wimbi la hivi karibuni la mauaji ya watu mashuhuri hususan tukio la Juni 8 la kuuawa kwa kupigwa risasi Mbunge wa Manispaa ya Arua Ibrahim Abiriga, walimwambia Museveni kwamba wamekuwa wakipokea vitisho vya kifo kupitia simu za mkononi na majukwa ya mitandao ya kijamii.
Habari zinasema Rais Museveni alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Ulinzi (CDF), Jenerali David Muhoozi, kukutana na Kamanda wa Polisi wa Bunge Mrakibu wa Polisi Anabella Nyamahoro kushughulikia mchakato wa kuongeza usalama wa wabunge. Nyamahoro alikuwa katika mkutano huo.
Wizara ya Fedha itatakiwa kukokotoa gharama za utaratibu huu wa maandalizi ya usalama.
Jenerali Muhoozi, Mkaguzi Mkuu wa Polisi, Martins Okoth-Ochola na Mkurugenzi wa Upelelezi (CID) Grace Akullo pia walihudhuria mkutano huo.
Vyanzo vya habari vinasema Rais aliagiza kwamba wabunge watakuwa wakisindikizwa na askari baada ya wabunge kuonyesha kutoridhishwa na walinzi wa kikosi cha polisi cha kupambana na ugaidi.
Wabunge, ambao waliunga mkono muswada wa marekebisho ya katiba uliopitishwa Desemba 2017 ili kuondoa ukomo wa umri wa rais, walipewa walinzi kutoka kikosi cha polisi cha kupambana na ugaidi kwani wapigakura waliokasirishwa na hatua hiyo walitishia kuwadhuru.
Mbunge wa Jimbo la Obongi, Hassan Kaps Fungaroo, ambaye alipuuza wito wa upinzani wa kususia na akahudhuria mkutano na Rais alisema wabunge wa chama tawala cha NRM walimwambia Rais Museveni kwamba wanapendelea kulindwa na UPDF badala ya polisi na pia waliomba magari ya kuwasindikiza.
"Kazi hii itafanywa zaidi na UPDF. Polisi waliokuwa wakiwalinda wabunge walikuwa wakikimbia (kwa sababu) walikuwa wanafikiria kazi ya kuwalinda wawakilishi wa wananchi ni hatari. Kwamba mazingira ya kazi yao (walinzi) ni hatarishi kwa maisha yao," alisema Fungaroo.
Walinzi hao watafanya kazi kwa muda wa miezi sita, kipindi ambacho Museveni anatarajia mapendekezo yake ya kuboresha usalama wa taifa yatatekelezwa.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad