MWENYEKITI mstaafu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) Patrobas Katambi amevituhumu vyama vya siasa vya upinzani kuwa huko nako kuna wanasiasa mafisadi na wabadhirifu wa fedha za umma.
Amesisitiza ni jambo la kushangaza pamoja na wanasiasa wengi wa vyama vya upinzani kuwa mafisadi bado wameendelea kunyoosha vidole kwa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wakati kwenye upinzani kuna ufisadi mkubwa unafanyika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Katambi ambaye kwa sasa ni kada wa CCM amesema kuna utafiti ambao umefanyika na kubaini kuna ufisadi mkubwa ambao unafanywa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani na anayo orodha ya wanasiasa 11 wanaongoza kwa ufisadi huo.
Katambi ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria amesema inasikitisha kuona jamii inakaa kimya wakati kuna wanasiasa wa upinzani wakiendelea kufanya ufisadi.“Tena baadhi yao wamekuwa wakijipambanua kuwa ni wazalendo na waadilifu lakini ukweli ndio wanaoongoza kwa ubadhirifu wa fedha za Watanzania.Ninayo majina 11 ya wanasiasa ambao wapo upinzani na wanaongoza kwa ufisadi.Kwa sasa sitataja majina yao ili wasivuruge ushahidi,”amesema Katambi.
Wakati anazungumzia wanasiasa hao wanaoongoza kwa ufisadi ameanza kwa kumtaja mwanasiasa namba moja kwa ufisadi nchini(akataja) huku akimtuhumu kwa kuonesha nyaraka mbalimbali.Amesema wanasiasa wa upinzani wamekuwa mstari wa mbele kunyoosha vidole pindi wanaposikia kuna masuala ya ufisadi au ubadhirifu wa fedha upande wa CCM na inapotokea upande wao wanakaa kimya.
Amesema uzuri wa CCM inapoona kuna mambo hayaendi sawa na kuna ubadhirifu au ufisadi eneo fulani wanachukua hatua kwa vitendo tofauti na upinzani ambao kuna wanasiasa wengi mafisadi lakini wanajifanya wasafi.
Hivyo ameomba haki itendeke pande zote na yupo tayari kwenda mahakamani iwapo anaowatuhumu watashindwa kuthibitisha tuhuma hizo huku akitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya mafisadi waliopo upinzani.
“Nchi yetu tumepewa na Mungu ,utajiri wa rasilimali za kila aina , ila watu wake ni masikini na nchi ni masikini kiuchumi.Sababu kubwa ni makosa ya aina ya siasa, mfumo na uongozi katika uamuzi , mipango , utekelezaji ,rushwa na mgongano kati ya maslahi binafsi na uzalendo (ufisadi),”amesema Katambi.
Ameongeza ugonjwa wa kukosa uzalendo na uaminifu ndio chanzo cha Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli kuamua kufanya uchunguzi na mabadiliko katika sheria , mifumo miundo na utendaji ili kuinusuru nchi yetu na taasisi washirika kiuchumi.
“Bila upendeleo wa utoaji taarifa ,vyombo vya habari kwa niaba na faida ya Watanzania leo wajue wapo mafisadi wakubwa kutoka vyama vya upinzani , walipata wapi uhalali na uhodari wa kuchambua na kutuhumu wenzao kwa ufisadi .“Sio vibaya nao Watanzania wakawajua na kutoa hukumu bila upendeleo ili kuisaidia nchi kupata viongozi wazalendo wa kweli,”amesema.