Mwenyekiti PAC Akalia Kuti Kavu Sakata la BoT

Mwenyekiti PAC akalia kuti kavu sakata la BoT
Mwenyekiti  wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka ameingia matatani baada ya kutoa majibu ya madai ya kuwepo kwa tuhuma za ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa vyombo vya habari kabla ya Spika.

Akijibu mwogozo ulioombwa na Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga amesema kitendo cha Mwenyekiti huyo wa PAC kuzungumza na vyombo vya habari kabla ya Spika Job Ndugai ni kinyume cha taratibu za Bunge.

Alisema suala la Mwenyekiti wa PAC kukiuka utaratibu litashughulikiwa na Spika Ndugai ambaye ndiye aliyeiagiza Kamati hiyo kufuatilia suala la tuhuma za BoT.

Kaboyoka ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki (Chadema), alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kile walichokibaini baada ya kuwahoji Bodi, Menejimenti ya BoT na Mlinga ambaye ndiye aliyetoa hoja hiyo bungeni wakati wa kuchangia Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Maofisa wa BoT akiwemo Gavana, Profesa Florens Luoga, walifikishwa mbele ya kamati hiyo baada ya Mlinga, kudai wametumia Sh bilioni 12 kwa matibabu ya watumishi wa benki hiyo nje ya nchi.

Mlinga alidai BoT ndiyo taasisi ya serikali inayotumia fedha nyingi kugharamia matibabu ya watumishi wake huku ukitumia kampuni binafsi ya bima badala ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

"Mpaka mtu kwenda kutibiwa nje kuna utaratibu na kuwe kuna haja ya kwenda kutibiwa nje. Hivi ninavyoongea watumishi wa BoT ndio taasisi inayotumia fedha nyingi katika matibabu bila msingi wowote.

" Mfanyakazi akiwa na mafua anakwenda kutibiwa India wanatumia fedha nyingi na wamesahau kuwa fedha hizi ni za walipa kodi.

Alisema taasisi za serikali zimewekewa utaratibu kwa ajili ya kupata matibabu kwa kutumia NHIF, lakini BoT wao wanatumia kampuni binafsi kwa gharama kubwa.

Alisema gharama ambayo wanatumia kwa ajili ya matibabu ambayo kama wangeitumia NHIF wangetumia Sh bilioni moja lakini wanatumia Sh bilioni 12 kwa mwaka kupitia kampuni binafsi ya bima na kuongeza kuwa huo ni ufisadi na wahusika wanafanya hivyo kwa maslahi binafsi.

"Wanasema NHIF haina matibabu ya nje kwa sababu wao ni taasisi nyeti lakini Usalama wa Taifa, Bunge, Takukuru, wako NHIF, Mke wa Rais aliugua na alilazwa Muhimbili lakini hata wabunge tumepima tezi dume kwenye zahati ya Bunge."

Baada ya hoja hiyo, Ndugai aliiagiza PAC inayoongozwa na Kaboyoka kufuatilia suala hilo kwa kuanza kukutana na Mlinga, NHIF, kisha kuiita Bodi na Menejimeti ya BoT na kumfikishia taarifa Jumatatu ya Juni 11, mwaka huu.

Baada ya kamati hiyo kufanya mahojiano na wahusika, Kaboyoka alinukuliwa na vyombo vya habari akizungumzia suala hilo na kudai kuwa tuhuma dhidi ya BoT hazina ukweli wowote kabla ya ripoti kuifikishwa kwa spika, kitendo kilichodaiwa na Mlinga kuwa ni kinyume cha kanuni za Bunge.

Hali hiyo ilimfanya mbunge huyo jana, baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu bungeni, kuomba muongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Giga.

"Mheshimiwa Mwenyekiti kamati zetu zinapoagizwa na Spika zifanye kazi, zinatakiwa zipeleke ripoti kwa Spika ndipo aitolee ufafanuzi.

"Mwishoni mwa wiki nilizungumza kuhusu BoT kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu kuliko taasisi nyingine za serikali ambazo zinafanya kazi ngumu. Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya PAC ikakaa na mimi, NHIF na BoT, taarifa nilizokuwa nazo hadi sasa Spika hajalitolea majibu suala hilo." Mlinga aliongeza:

"Lakini jana (juzi) nimeona kwenye taarifa ya habari Mwenyekiti wa Kamati ya PAC akitoa taarifa za kamati ambayo ni siri mpaka Spika atakapotolea majibu, akisema taarifa kuhusu BoT kutumia fedha nyingi kwenye matibabu si za kweli.

"Mheshimiwa Spika naomba kupatiwa utaratibu kama na mimi naweza kulizungumzia suala hilo kwenye vyombo vya habari, kwani hata mimi nilizongwa zongwa na vyombo vya habari, lakini niliheshimu kanuni," alisisitiza Mlinga.

Baada ya kuomba muongozo huo, Mwenyekiti Giga alisema suala hilo ni kinyume cha kanuni na Spika atalishughulikia. "Na wewe Mlinga usizungumze na vyombo vya habari kwani ukifanya hivyo, utakuwa umekiuka kanuni za Bunge."
==

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad