Maneno yenye kuandikwa au kutamkwa yanaweza kusababisha matokeo makubwa na kutengeneza kumbukumbu inayishi muda mrefu, ambayo inaweza kuwa mbaya au nzuri. Hivyo, ni muhimu kutumia busara katika kuchagua maneno ya kuzungumza au kuandika. Maneno huvunja uhusiano, vilevile yanaweza kumjenga mtu au kumbomoa.
Nukuu ambayo hupatikana kwenye shairi moja la Kiingereza husema: “Words are seeds that do more than blow around. They land in our hearts and not the ground. Be careful what you plant and careful what you say. You might have to eat what you planted one day.”
Tafsiri yangu: Maneno ni mbegu zenye kuzaa zaidi kuliko kuyeyuka. Hutua mioyoni mwetu na siyo ardhini. Kuwa makini na kile unachokipanda na uwe makini kwa ukisemacho. Siku moja unaweza kulazimika kula ulichopanda.
Huu ni mwaka wa tatu tangu mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alipotoa kauli ya “bao la mkono”, alipokuwa akiweka msisitizo kwamba chama chake (CCM) kingepata ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu 2015 iwe isiwe. Alisema hata ingebidi basi wangefunga kwa goli la mkono.
Kwa wapenzi wa soka waliokuwepo au wanaofuatilia historia, ukiwaambia goli la mkono, kwa haraka zaidi wanakumbuka tukio la Juni 22, 1986. Siku hiyo shujaa wa soka wa wakati wote wa Argentina na duniani kote, Diego Maradona, alifunga bao la mkono katrika dakika ya 51 dhidi ya England, kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
Goli hilo liliwaumiza mno England, kwani lilikuwa moja kati ya mawili yaliyofungwa na Maradona na kuwaondoa England na kuivusha Argentina kwenda nusu fainali, kisha fainali ambako iliifunga Ujerumani Magharibi na kuchukua Kombe la Dunia kwa mara ya pili.
Bao hilo la mkono ambalo hufahamika zaidi kama Goli la Mkono wa Mungu, liliwaumiza England si kwa sababu ya kutolewa robo fainali, bali mechi hiyo ilikuwa muhimu kushinda, kwa kuwa ilikuwa imepita miaka minne tangu Argentina na Uingereza zipigane vita ya Falklands ambayo ilitokana na mgogoro wa Kusini ya Bahari ya Atlantic mwaka 1982.
Dakika ya 55 ya mchezo, Maradona alifunga bao murua sana, akiwapiga chenga na kuwakokota wachezaji watano wa England na kipa wao wa sita kisha akaweka mpira nyavuni. Bao hilo la pili lilipewa hadhi ya kuwa “Goli la Karne ya 20”, hata hivyo, England hawalikumbuki hilo, bali lile la Mkono wa Mungu.
Kimsingi goli la mkono ni faulo. Na kwa sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ukibainika umefanya mchezo kama wa Maradona lazima uadhibiwe kwa kadi.
Hivyo, Nape alipotangaza kuwa CCM ingeshinda hata kwa bao la mkono, alikuwa akiutangazia umma kwamba chama hicho kilidhamiria kushinda uchaguzi kwa mbinu zozote, ziwe halali au haramu.
Lilikuwa tangazo baya, ingawa kwa ubongo usiopenda kuhukumu, ni rahisi kuamini kwamba Nape alizidiwa na hisia kuelekea kipindi cha kampeni.
Nyakati kama hizo, mambo mengi husemwa, uropokaji huwa mwingi. Kila mmoja hujaribu kunena lile lenye faida upande wake na kuumiza ule wa pili.
Nyakati hizo pia au vipindi vyenye joto kali la uchaguzi, mara nyingi ustaarabu huwa mdogo. Hivyo unaweza kuyaona maneno ya Nape kuwa yalitoka katika mazingira ya hisia za uchaguzi. Mazingira ambayo kwa kawaida hutawaliwa na asilimia chache za uungwana.
Hata hivyo, kwa kauli yake hiyo, sasa anajikuta analipia gharama kama mtu binafsi na siyo chama. Kipindi kile alikuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi. Ndiye alibeba wajibu wa kuisemea na kuitetea CCM. Hivi sasa Nape si kiongozi CCM wala Serikali aliyoinadi kuwa ingepatikana hata kwa bao la mkono. Ni mbunge tu.
Juni 11, mwaka huu mtandao wa Jamiiforums ulisitisha kutoa huduma. Uongozi wa mtandao huo ulitoa tangazo kwamba ulilazimika kuondoka hewani ili kutii agizo la Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), lililotaka mtandao huo usiendelee kutoa huduma kuanzia Juni 11.
Nape alikuwa mmoja wa waliotoa maoni yao kupitia mtandao wa Twitter, akikosoa kwamba kuifungia Jamiiforums ni kuminya uhuru wa habari na haki ya kutoa maoni.
Kauli hiyo ilisababisha kuibuka kwa watu ambao walimshambulia katika maeneo mawili; mosi ni kauli yake ya bao la mkono, pili ni kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari mwaka 2016.
Mwaka 2016, Nape akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alipeleka bungeni muswada huo ambao ulilalamikiwa mno kwamba ulijaa ukandamizaji kwa tasnia ya habari. Wadau wengi walishauri muswada huo ucheleweshwe kwanza ili ufanyiwe marekebisho.
Pamoja na sauti za wengi, hasa wadau, waziri mwenyewe wa habari, Nape alipeleka muswada huo bungeni na wabunge waliupitisha, kisha Rais John Magufuli aliusaini ili uwe sheria.
Kwa kitendo hicho, Nape baada ya kukosoa Jamiiforums kufungiwa, watu walimkumbusha uhusika wake kwenye Sheria ya Huduma za Habari.
Walijitokeza wengine waliomwambia kwamba kufungiwa kwa Jamiiforums si tukio la kutisha kama bao la mkono. Wakaenda mbele zaidi na kueleza kwamba hatua ya sasa hadi yeye (Nape) anaona uhuru wa habari na utoaji wa maoni unaminywa ni matokeo ya bao la mkono.
Baada ya Nape kuona mashambulizi yamekuwa mengi, aliamua kujibu kwa kuandika kwamba alaumiwe kwa “bao la mkono” na siyo kufungiwa kwa Jamiiforums.
Kauli hiyo ikazidi kuamsha mashambulizi dhidi yake, kwani wengi maoni yao ni kama walitafsiri kuwa Nape anajutia kosa la utekelezaji wa bao la mkono kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.
Nape alilazimika tena kurejea mtandaoni na kutoa ufafanuzi kuwa anakubali kulaumiwa kwa kutamka kauli yake ya “bao la mkono”, akaeleza kuwa hakuna mahali ambako anajua bao la mkono lilitumika, akaongeza kwamba yeye mwenyewe jimboni alishinda kwa mapambano makali. Anaomba radhi na suluhu, akitaka watu waweke silaha chini.
Aliandika Twitter: “Naomba turudishe visu vyetu kwenye ala; namaanisha nilaumiwe mimi kwa kuasisi usemi wa bao la mkono mwaka 2015. Sijui na siamini kama kuna aliyefunga bao la mkono mwaka 2015. Mimi mwenyewe nilibanwa Mtama kampeni nzima na kuponea chupuchupu. Rudisheni visu kwenye ala.”
Jinsi Nape anavyojitetea inaturejesha kwenye lile shairi la Kiingereza, kwamba maneno ni mbegu inayoweza kustawisha mazao kuliko kuyeyuka. Mbegu ya maneno huwa haipandwi ardhini bali mioyoni. Ndiyo maana watu wanatokeza sasa wanamshambulia Nape ni kwamba kauli yake ya bao la mkono iliingia ndani kabisa kwenye nyoyo zao.
Gwiji wa siasa za Tanzania, Thabit Kombo aliacha maneno ya hekima kwamba ni vizuri watu wakawa na utaratibu wa kuweka akiba ya maneno.
Kama ambavyo watu wanamsuta Nape kwa kauli yake ya bao la mkono, ndivyo na wasutaji kwa wakati wao wanaweza kusutwa kwa maneno yao. Ni vizuri kuweka akiba ya maneno.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, viongozi wa Chadema walipitia kipindi cha kubanwa na maswali mengi kuhusu uamuzi wao wa kumpokea Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kutoka CCM na kumteua kuwa mgombea urais, wakati walikuwa wa maneno mengi ya kumsema vibaya kwamba ni fisadi.
Viongozi wa Chadema, kama ilivyokuwa kwa Nape kipindi akiwa katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, walikuwa sawa na mwamba ngoma, kwa hiyo wakawa wanavutia kwao.
Kulikuwa na dalili kuwa Lowassa angekuwa mgombea urais wa CCM, na kutokana na nguvu zake kisiasa, angewapa taabu sana wapinzani.
Hivyo, wapinzani kwa kutambua hilo, waliamua kumshughulikia Lowassa kwa maneno ya kila aina. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kwamba chama chake kisingekuwa tayari kupokea makapi, akimaanisha wale ambao wangekatwa kwenye mchakato CCM, wasingepewa nafasi Chadema.
Kulikuwa na faida kubwa upande wao kwa maneno yao kulingana na wakati ambao Chadema walikuwa wanapitia. Ilikuwa lazima wajitengenezee barabara rahisi ya kupita kuelekea uchaguzi ambao chama chao kilikuwa kinakwenda kupambana na chama kikubwa zaidi, kilichokuwa na dalili ya kumsimamisha mgombea mwenye ushawishi mkubwa.
Hasara mbili kwa Chadema kipindi wakitapatapa huko kwa maneno ni kwamba hawakuweka akiba ya maneno. Pili, maneno yao yalikuwa mbegu ndani ya mioyo ya watu. Matokeo ya hasara hizo ni kuifanya CCM ipate mteremko wa kuishambulia Chadema kipindi cha kampeni baada ya kumpokea Lowassa.
Hoja ilikuwa moja tu, kwamba “walisema ni fisadi mbona amewanunua?” Suala la Chadema kununuliwa na Lowassa yalikuwa ni maneno yenye kufyatuka wakati wa kampeni.
Kwa Chadema yalikuwa magumu kuyatolea majibu kwa sababu ya historia ya matamshi yao kwa Lowassa na walivyompokea. Walisema ni fisadi, wakaahidi kutopokea makapi kutoka CCM. Mbona Lowassa alipokelewa? CCM wakasema aliwanunua.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alipitia kwenye wakati mgumu wakati wa kampeni mwaka 2015, sababu ya kauli yake kwamba ambaye angemuunga mkono Lowassa apimwe akili.
Msigwa alilazimika kukiri kuwa alikosea kutamka kauli hiyo kwenye mdahalo wa wagombea ubunge Iringa Mjini. Maana Lowassa alikuwa mgombea urais wa chama chake.
Mwisho ni ushauri kwa Nape, kutambua kuwa maneno ni kama binadamu, akishazaliwa, hata akifa ataitwa marehemu, yaani alikuwapo ila Mungu alimchukua. Maneno yakishatamkwa, hata ukiyakana, ukiyatolea ufafanuzi au kuomba radhi, hayawezi kufutika.
Binadamu na nongwa zao, wakishayaweka mioyoni, ipo siku watakumbusha tu. Ushauri kwa Nape ni kujitahidi kubaki kama kiongozi. Inafahamika bao la mkono ni maneno yaliyofyatuka katika kipindi cha kuelekea kampeni. Si sawa kipindi hiki kubishana na watu.
Hata ajitetee vipi, binadamu kwa nongwa zao watamsuta tu. Anachotakiwa kufanya ni kukaa kimya, maana ukimya ni busara, kusema sana na kutaka kujibu au kujitetea kwa kila kitu ni kupungukiwa sifa ya uongozi. Je, ni nani asiyekosea?