Nape Kuungana na Zito Kabwe Kupinga Sheria Mpya ya Korosho


Serikali inakusudia kuifanyia marekebisho Sheria ya Sekta ya Korosho namba 203.

Kwa mujibu wa muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2018, inapendekezwa kufutwa mgawo wa fedha zinazotokana na ushuru wa kusafirisha korosho nje zilizokuwa zikitolewa kwa wakulima ili kuboresha zao hilo.

Badala yake, muswada unapendekeza fedha hizo kupelekwa mfuko mkuu wa Hazina kama fedha nyingine za Serikali.

Sheria ya sasa inataka asilimia 65 ya fedha zinazotokana na ushuru wa kusafirisha korosho nje kupelekwa kwa wakulima kupitia Bodi ya Korosho (CBT).

Fedha hizo zilikuwa zikitumika kuendeleza kilimo cha korosho kama vile kuendesha Chuo cha Utafiti Naliendele, kufanya utafiti wa mbegu bora na kuzuia magonjwa ya mnyauko.

Muswada unapendekeza kifungu cha 17A kibadilishwe kwa kufuta kifungu kidogo cha (2) na kuingizwa kipengele kipya.

Kifungu kipya kinachopendekezwa kinasomeka, “Mapato yote yatokanayo na ushuru wa kusafirisha korosho yatahifadhiwa katika mfuko mkuu.”

Hivi karibuni wabunge waliibana Serikali wakitaka kujua ziliko fedha zinazotokana na mapato ya ushuru wa usafirishaji wa korosho nje.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia alitaka majibu ya Serikali, akisema ripoti zinaonyesha fedha hizo zilizokusudiwa kuendeleza kilimo cha korosho zimetumika katika matumizi mengine.

“Kukubali mapendekezo haya ya mabadiliko ya sheria hii ni kuhujumu juhudi za miaka mingi za kufufua zao la korosho, ni kuwatoa kafara wakulima wa korosho nchini na kuhujumu mapato ya Serikali kwani korosho ndiyo zao lililofanya vizuri msimu uliopita. Nitayapinga," amesema Nape katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad