NIGERIA na Argentina leo zina kazi ngumu ya kupenya hatua ya 16 ya michuano ya Kombe la Dunia, kila moja ikihitaji ushindi kufuzu hatua hiyo.
Timu hizo zinakutana leo katika mechi inayotarajiwa kuwa na msisimko na inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani, kutokana na matokeo ya mechi zilizopita kwa timu hizo.
Waafrika wana matumaini makubwa kwa Nigeria kufuzu hatua hiyo wakitarajia itatumia vizuri udhaifu wa Argentina ulioonekana katika mechi mbili zilizopita ambapo ilitoka sare na Iceland kabla ya kuchapwa mabao 3-0 na Croatia.
Nigeria inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D ikiwa na pointi tatu nyuma ya Croatia inayoongoza kwa pointi sita baada ya kushinda mechi zake zote mbili za mwanzo.
Argentina ipo mkiani ikiwa na pointi moja sawa na Iceland iliyo nafasi ya tatu. Ili timu iwe salama katika kufuzu hatua ya 16 bora, inahitaji ushindi katika mechi ya leo, Argentina ikishinda itafikisha pointi sita na hivyo itakata tiketi ya kufuzu hatua hiyo, lakini ikiruhusu Argentina ishinde, itaaga michauno hiyo.
Argentina na Nigeria zinafahamiana kwenye michuano hiyo, si tu kwamba zimeshacheza mara nne kwenye kombe la dunia, lakini zilikutana kwenye faunali za Olimpiki mwaka 2008 na Argentina kushinda bao 1-0.
Wachezaji wanne wa kikosi kile cha Argentina bado wapo kwenye kikosi kilichokwenda Urusi, Lionel Messi, Javier Mascherano, Sergio Aguero, na Angel Di Maria, aliyefunga bao la ushindi Beijing. Kocha wa Nigeria Gernot Rohr alikizungumzia kikosi chake chenye wachezaji chipukizi.
"Kama una timu yenye wachezaji chipukizi unapaswa kuwa mtulivu na kukubali makosa yatakayotokea kwa sababu ni sehemu ya mchezo. Hata katika mechi yetu ya kwanza na ya pili niliona vitu vya kufanyia kazi, timu itakuwa sawa katika mechi ya tatu.”
“Tunatakiwa kuyashinda magumu, tunatakiwa kuchukia kwa kile kilichotokea katika mechi zilizopita ni lazima tupambane tushinde,” alisema Javier Mascherano kwenye mahojiano na FIFA.