Wawakilishi wa Afrika kwenye kinyang’anyiro cha Kombe la Dunia 2018 timu ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ leo jioni itashuka dimbani katika mchezo muhimu watakaolazimika kucheza kufa au kupona kupata matokeo.
Nigeria iliyo kundi D itaivaa Iceland, ikiwa na kumbukumbu za kupoteza mchezo wa kwanza kwa kupigwa mabao 2-0 na Croatia, hivyo kipigo katika mchezo wa leo kitaifanya iyaage mashindano hayo.
Kwa kujua hilo Kocha Gernot Roh, atalazimika kukipanga vema kikosi chake baada ya kuiona Iceland inayoshiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia, ikionyesha kuwa imekuja kushindana na sio kushiriki baada ya kuibana Argentina na kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Mbali ya mechi hiyo pia kuna mchezo unaosubiriwa kwa hamu wa kundi E, utakaopigwa leo saa 9:00 alasiri kati ya Brazil iliyoanza fainali za mwaka huu kwa sare dhidi ya Uswisi, itaikabili Costa Rica na baaye utapigwa mchezo kati ya Serbia na Uswisi saa 3:00 usiku.
Brazil nayo itashuku dimbani ikifahamu fika kuwa Costa Rica iliyo jeruhiwa katika mchezo uliopita kwa kupigwa bao 1-0 na Serbia, itashuka dimbani kama Nyati aliyejeruhiwa ikisaka ushindi kwa udi na uvumba.
Kutokana na hilo na kile kilichowakuta majirani zao Argentina jana walipopokea kichapo cha kustusha cha mabao 3-0 kutoka kwa Croatia, ni wazi kuwa kutakua na patashika dimbani.