Msanii wa muziki wa kizazi kipya Nikki wa Pili, amesema ‘kiki’sio kigezo pekee cha msanii kufanikiwa katika soko la muziki wa sasa, bali kuna mambo mengi ya kisanaa anayopaswa kuyafuata ili aweze kufikia malego yake.
Nikki ametoa kauli hiyo baada ya mtayarishaji mkongwe wa muziki Master J, kusema kwamba soko la muziki wa sasa linahitaji msanii afanye kiki ili aweze kufanikiwa katika tasnia hiyo.
Nikki ameeleza kuwa kuna sababu nyingi zinazo mpelekea msanii kufanikiwa ikiwa ni pamoja na wimbo na video ya muziki aliofanya, lakini pia uhusiano wa msanii na vyombo vya habari na vilevile uwezo wake kifedha.
“Sio kweli kwamba kiki ndo ina mfanikisha msanii, mbona kuna wasanii wengi tuu wamefanikiwa bila hizo kiki na video zenye utupu, kwa mfano sisi weusi tumefanya muziki kwa muda mrefu na kufanikiwa bila hayo mambo”, amesema Nikki.
Nikki wa Pilli ni moja kati ya wasanii wanaounda kundi la muziki la Weusi, ambapo wengine ni Gnako, Joh makini na Bonta.