Oparesheni Kata Umeme Nchi Nzima Kuanza Kesho

Tanesco Yawatangazia Kiama Wadaiwa Sugu
SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limetangaza operesheni kata umeme nchi nzima kwa wadaiwa sugu kuanzia kesho.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa katika gazeti la Nipashe mwishoni mwa wiki, ukataji wa umeme huo utahusisha taasisi za serikali na za watu binafsi, mashirika ya umma, viwanda na majumbani.

Operesheni hiyo itaanza rasmi kesho kwa Tanesco kusitisha huduma kwa wateja wote wanaodaiwa malimbikizo ya madeni ya ankara za umeme.

"Wateja wote wenye madeni wanatakiwa kulipa bili zao kabla ya Juni 26, mwaka huu (kesho). Tanesco haitatoa taarifa nyingine zaidi ya tangazo hili," lilisema tangazo hilo.

Machi mwaka jana, Rais John Magufuli alisema taasisi zote za umma zinapaswa kulipwa madeni ya Tanesco la sivyo zitakatiwa umeme.

Rais Magufuli aliyekuwa akiweka jiwe la msingi kwenye kituo kipya cha Tanesco mkoani Mtwara, alisema Serikali ya Zanzibar kupitia Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), ina deni la Tanesco la kiasi cha Sh. bilioni 121.

"Msiogope mnapaswa kukata huduma hii kwa taasisi yoyote ambayo hailipi bili zake. Nataka kumwambia Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (wakati huo) kwamba umeme unapaswa kukatwa hata Ikulu. Nikilala gizani, halafu maofisa wa Ikulu ambao hawajalipa watawajibika na siyo wewe. Una hakikisho langu kwa hili," alisisitiza.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad