Pesa Zateketea Mkutano wa Trump, Kim Watafuna Shilingi Bilioni 45

Hela Zateketea Mkutano wa Trump, Kim Watafuna Shilingi Bilioni 45
Gharama za mkutano wa kilele kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ulipangwa kugharimu dola za Marekani 20 milioni (Sh 45 bilioni), Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumapili Lee alisema, “Ni gharama ambazo tuko radhi kulipa.” Lee aliongeza huo ni mchango wao katika masuala ya kimataifa na kwamba yote ni kwa “masilahi makubwa” ya Singapore.

Waziri mkuu huyo alisema nusu ya fedha hizo zilipangwa kutumika kwa ajili ya masuala ya usalama ikijumuisha walinzi 12 wa Kim Jong-un waliokuwa wakikimbia kando ya gari lake kutoka uwanja wa ndege hadi kwenye eneo la mkutano.

Lee alieleza kwamba kutokana na mazingira ya mkutano huo kuhusisha maofisa wa ngazi ya juu, mahitaji ya usalama pia yalikuwa makubwa kuliko matukio mengine yote ya kisiasa.


Mbali ya uwepo wa idadi kubwa ya maofisa wa polisi, maofisa usalama walihusika “kulinda maeneo yote na kwa kina – ulinzi wa nga, baharini na ardhini – dhidi ya uwezekano wa shambulio lolote au tukio lolote la bahati mbaya.”

Gazeti la Kiingereza la Straits Times la Singapore lilinukuu chanzo kutoka Wizara ya Habari na Mawasiliano ikisema kiasi cha dola 5 milioni (Sh 11.376 bilioni) zilitumika kwa ajili ya kituo kwa wanahabari katika jengo la F1 Pit Building.

Kiasi kilichosalia kilipangwa kutumika kwa ajili ya malazi ya wanahabari wapatao 2500 kutoka pande mbalimbali za dunia na pia maofisa waliokuwa katika msafara wa Trump na Kim.

Viongozi wawili hao – Trump akitokea katika taifa kubwa kiuchumi na demokrasia na Kim akitokea taifa lisilo na maendeleo makubwa – waliwasili Singapore Jumapili; walikutana ana kwa ana kabla ya kuwa pamoja na washauri wao kisha wakapata chakula cha pamoja.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad