Pingamizi la Mbowe na Viongozi Chadema Latupiliwa Mbali Mahakamani

Pingamizi la Mbowe na Viongozi Chadema Latupiliwa Mbali Mahakamani
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali pingamizi la viongozi wa CHADEMA akiwemo Freeman Mbowe la kutaka kesi ya kufanya maandamano ifutwe badala yake imeagiza hati ya mashtaka ibadilishwe.

Hata hivyo, upande wa utetezi kupitia wakili wa Peter Kibatala, umetangaza nia ya kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambapo amesema anakubaliana na hoja 2 za upande wa mashtaka kati ya hoja zao 8 za pingamizi.

Katika kesi hiyo pingamizi kuu la upande wa utetezi wameiomba mahakama hiyo ifute kesi hiyo kwa sababu baadhi ya mashtaka ni batili.

Katika uamuzi wake Hakimu Mashauri amesema hakuna haja ya kesi hiyo kufutwa badala yake anaagiza upande wa mashtaka uifanyie marekebisho hati ya mashtaka.

Hata hivyo, wakili Kibatala amedai kuwa wanatangaza nia ya kukata rufaa kwa sababu kama mahakama imeona mashtaka hayo ni batili kwanini isingeyafuta badala yake imeagiza yabadilishwe.

Upande wa mashtaka kupitia Wakili wa serikali Mkuu, Paul Kadushi umedai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama za Mahakimu hakuna uwezekano wa kukata rufaa katika uamuzi mdogo ambao hauwezi kuathiri kesi.

“Naomba mahakama ipuuzie hoja hizo na nia hiyo ni batili,”ameeleza Kadushi.

Kutokana na mvutano huo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi June 12,2018 ili kutoa uamuzi kama upande wa mashtaka ukate rufaa ama lah.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika.

Mbunge wa Tarime mjini Esterher Matiko, Katibu wa chama hicho Dk Vicenti Mashinji, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, mbunge wa Tarime vijijini, John Heche na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali ama maandamano yaliyosababisha kifo cha Akwilina.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad