Polepole Aisifu Barua ya Maaskofu, Serikali Yaikana

Polepole Aisifu Barua ya Maaskofu, Serikali Yaikana
Wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akiisifu barua waliyoandikiwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakitakiwa kuufuta waraka wa Pasaka ndani ya siku kumi, Serikali imesema barua hiyo ni batili.

Ufafanuzi wa Serikali kuhusu barua hiyo umetolewa leo Ijumaa Juni 8, 2018 na waziri wa wizara hiyo, Dk Mwigulu Nchemba katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Wakati leo Mwigulu akieleza kuwa taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni batili na sio maelekezo ya serikali au wizara, Polepole kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter alionekana kuunga mkono tamko la Serikali lililokanushwa na Dk Mwigulu.

Hata hivyo, baada ya barua ya msajili kusambaa katika mitandao ya kijamii, Polepole kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika ujumbe wenye tafsiri ya kukubaliana na kilichoandikwa.

“Serikali makini ina wajibu wa kukumbusha, kuelekeza, kuonya au kuchukua hatua kwa mtu au taasisi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu za nchi ambazo tumejiwekea,” ameeleza Polepole aliyekuwa katika majibizano na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.

Dk Mwigulu amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hivyo akawataka viongozi wa dini waendelee na kazi zao.

Kufuatia tamko hilo batili, waziri huyo amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kiraia, Merlin Komba.

Waziri Mwigulu amesema serikali ikiwabaini waliotengeneza barua hiyo feki itawachukulia hatua za kisheria huku akionya watu wanaotaka kucheza na amani na nchi.

Pia, jana Juni 7, 2018 baada ya kusambaa kwa barua ya KKKT kwenda kwa msajili wa vyama, ikieleza ufafanuzi wa mambo waliyotakiwa kutekeleza, Polepole aliandika tena katika ukurasa wake wa Twitter;

“Kama hii ni kweli, ni ukomavu wa juu kabisa kiuongozi. Kwa awali kuwapongeza KKKT, niliumia moyo ibilisi alitaka kutumia pungufu hili kuleta mfarakano usiokuwepo, tumemshinda. Wale walifanya press conference (mkutano na waandishi wa habari) kwa barua hii waitishe press nyingine. Mzee wa kujichomeka hapa imekwama,” ameandika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad