Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuendelea kuwa watumishi wa watu kwa kufikika kwa haraka pale wanapohitajika ikiwa ni pamoja na kusimamia mali za Umma na Chama hicho kwa kuwa ndio msingi wa ushindi wa CCM katika zama zote.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Bw. Humphrey Polepole wakati akiwa amekutana na Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wa Majimbo, Wilaya na Mikoa yote ya Zanzibar na kuendesha Mafunzo ya Kimkakati ya kuwaongezea maarifa, uweledi na ujuzi katika eneo la Siasa, Itikadi na Uenezi.
Polepole amesema kwamba zile zama za viongozi kujihisi wako juu ya wananchi na hawawezi kupatikana pale wanapohitajika na wananchi zimekwisha, na kwamba Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pi ni rais wa nchi yeye anawapatia fursa wananchi wake pale wanapomuhitaji.
"Zama za viongozi kuwa Mungu watu zimekwisha kwenye chama chetu, ukipigiwa simu pokea. Ukitumiwa meseji jibu hata kama hutaweza kujibu meseji zote. Mimi najua Mwenyekiti John Pombe Magufuli anapokea simu na anajibu meseji, wewe waziri ni nani au wewe kiongozi wa Chama mkoa hufikiki umekuwa nani? Zama hizo ndani ya CCM hakuna tena nawataka mjirekebishe," Polepole
Pamoja na hayo Katibu Mwenezi huyo amewataka wanaCCM kupitia vikao kuendelea kuifuatilia, kuisimamia na kuitathimini Serikali yao katika namna ambavyo itaendelea kuchochea maendeleo ya wananchi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015-2020.