Rais Mnangagwa Kukutana na Magufuli Leo Hapa Nchini

Rais Mnangagwa Kukutana na Magufuli Leo Hapa Nchini
Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, atafanya ziara nchini leo na kesho, huku masuala ya kiuchumi yakitazamwa zaidi katika ziara hiyo.

Ziara hiyo ni ya kwanza Tanzania tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana.

Anafanya ziara ikiwa ni siku chache tangu aliponusurika kifo baada ya bomu kulipuka wakati akimalizia mkutano wa kampeni katika mji wa Bulawayo nchini humo.

Rais Mnangagwa alinusurika baada ya mlipuko kutokea kwenye mkutano huo huku wasaidizi wake wakiwamo makamu wake wawili na viongozi wa chama wakijeruhiwa.

Uchaguzi mkuu wa Zimbabwe unatarajiwa kufanyika Julai 30 kumchagua Rais na wabunge wa mabunge mawili.

Mambo ya ushirikiano

Ziara ya kiongozi huyo inakuja wakati Taifa hilo na Tanzania yakiwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kisiasa na kiuchumi.

Kisiasa, Tanzania ilikuwa nchi pekee kusini mwa Afrika iliyojitoa kuanzisha harakati za ukombozi wa nchi nyingi zilizo upande huo wa bara, kujikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni.

Kutokana na uamuzi huo uliofanyika chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wapigania uhuru wa mataifa hayo ikiwamo Zimbabwe walipatiwa hifadhi hapa nchini, mbinu za kijeshi na kiharakati za kupigania uhuru.

Vilevile walipatiwa vifaa na kuwezeshwa katika mambo mengine waliyohitaji. Zimbabwe ilipata uhuru wake Aprili 18, 1980.

Kwa upande wa kiuchumi, Zimbabwe yenye watu milioni 16.2 (kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2016) inaitumia Bandari ya Dar es Salaam katika usafirishaji wa mizigo na bidhaa nje ya Afrika na upokeaji wa mizigo yake.

Taifa hilo lisilo la bahari, limekuwa likiitumia bandari hiyo kwa miaka mingi, ingawa pia bidhaa zake nyingine hupitia katika nchi ya Msumbiji.

Lengo la ziara

Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje, ilisema lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha kwa rais huyo kwa wananchi wa Tanzania.

Tangu aingie madarakani, Mnangagwa ameshafanya ziara Namibia, Zambia, Msumbiji, Angola, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Botswana.

Wizara hiyo ilisema ziara hiyo ni muhimu kwa Tanzania kwa kuwa itatoa fursa ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano uliopo wa kidiplomasia, kihistoria, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizi mbili.

Mbali ya ushirikiano huo wa kiserikali, chama cha Zanu-PF kinachoongoza Zimbabwe kina ushirikiano na CCM.

Ziara hiyo pia itatoa fursa kwa viongozi kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi.

Rais Mnangagwa atafanya mazungumzo na Rais John Magufuli na atatembelea Chuo cha Sanaa cha Kaole Bagamoyo ambacho awali kilitumika kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Afrika. Mnangagwa ni miongoni mwa waliopata mafunzo katika chuo hicho.

Wasifu wake

Mnangagwa amekuwa akiitwa ‘Garwe’ au ‘Ngwena’, ikimaanisha mamba kwa lugha ya Kishona kwa sababu lilikuwa ni jina la jeshi la msituni alilolianzisha, lakini baadaye ikawa ni nguvu zake kisiasa.

Kundi linalomuunga mkono ndani ya Zanu-PF linaitwa Lacoste kutokana na kampuni ya Kifaransa nchini humo yenye nembo ya mamba.

Mnangagwa alizaliwa Septemba 15, 1942 ni Rais wa Zimbabwe aliyeingia madarakani Novemba 24, 2017 baada ya jeshi la nchi hiyo kumuondoa Robert Mugabe aliyeitumikia nchi hiyo tangu akiwa waziri mkuu mwaka 1980.

Mnangagwa aliyekuwa makamu wa Mugabe na mwanachama mkongwe wa Zanu-PF alishika wadhifa huo tangu mwaka 2014 hadi aliposimamishwa Novemba 2017 na kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini kabla ya kurejeshwa na jeshi kushika madaraka.

Hata hivyo, Umoja wa Afrika (AU)haukuyaita mapinduzi, bali matakwa ya wananchi wa Zimbabwe.

Mnangagwa alikuwa mpiganaji wa msituni tangu wakati wa utawala wa kikoloni wa Rhodesia. Baada ya Zimbabwe kupata uhuru alishika nafasi kadhaa za uwaziri chini ya Mugabe ikiwa ni pamoja na waziri wa Nchi wa Ulinzi hasa wakati wa mauaji yanayofahamika kama Gukurahundi ambapo takriban watu 20,000 wengi wakiwa wa kabila la Ndebele waliuawa.

Kiongozi huyo alililaumu jeshi kwa kuhusika na mauaji hayo, huku akiendelea kushika nafasi za juu katika baraza la mawaziri. Mwaka 2005 alishushwa cheo na kuwa waziri wa Makazi Vijijini baada ya kutania waziwazi kuwa anataka kurithi kiti cha Mugabe, lakini mwaka 2009 alirejea nafasi za juu.

Baada ya uchaguzi wa 2009, Mnangwaga alikubaliana kugawana madaraka na Rais Mugabe na kupewa uwaziri wa Ulinzi kuanzia mwaka 2009 hadi 2013 alipoteuliwa kuwa waziri wa Sheria kabla ya kuteuliwa kuwa makamu wa Rais mwaka 2014 na alitarajiwa kuwa mgombea urais baada ya Mugabe.

Hata hivyo, alikuwa akipingwa na kundi la G40 (Generation 40) lililokuwa likiongozwa na mke wa Mugabe (Grace). Kundi hilo ndani ya Zanu-PF lilikuwa la kizazi cha vijana waliokuwa wakiwapinga viongozi wazee ndani ya chama hicho.

Mwanzoni mwa Novemba 2017, Mnangagwa aliondolewa kwenye umakamu wa Rais akituhumiwa kutaka kuipindua Serikali na kukimbilia Afrika Kusini alikokaa kwa wiki mbili. Mshirika wake mkubwa ambaye alikuwa mkuu wa Jeshi la Zimbabwe, Jenerali Constantino Chiwenga alianzisha mapinduzi akimuweka kizuizini Mugabe katika makazi yake yaliyopo nje ya Ikulu ya nchi hiyo.

Chiwenga pia aliwakamata viongozi juu wa Zanu-PF na hapo ndipo Mnangagwa aliporejea kutoka Afrika Kusini na kushika nafasi ya Mugabe.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad