Rais wa Ufilipino Amtukana Mungu Amwita Mpumbavu

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amemwita Mungu "mpumbavu", hatua ambayo imekera sana watu katika taifa hilo lenye Wakatoliki wengi.

Kiongozi huyo amesema hayo kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.

Aidha, amekosoa vikali hadithi ya Adam na Hawa kuhusu jinsi walivyotenda dhambi na kuondolewa kutoka kwenye neema ya Mungu.

Kadhalika, amekosoa wazo kwamba kila binadamu tangu wakati huo huzaliwa akiwa na dhambi asilia.

Bw Duterte anajulikana sana kwa matamko yake yenye kuzua utata pamoja na matusi yenye kutumia lugha kali dhidi ya wapinzani wake.

Ingawa kanisa na raia wamemshutumu kwa hilo, afisi ya rais huyo imesema alikuwa tu anaeleza imani yake binafsi.

Rais huyo amewahi kumshutumu pia Papa kwa kutumia maneneo makali na ana historia pia ya kuwatusi viongozi wengine.

Tamko la sasa alilitoa katika hotuba mji wa Davao, mji ambao alikuwa kiongozi wake kabla ya kuwania urais.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad