Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto anaendelea kuwakosesha usingizi wapinzani kwa kunyemelea ngome zake za kihistoria huku akijitayarisha kuchukua uongozi wa nchi kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta miaka minne kuanzia sasa.
Ruto amekuwa akizuru maeneo ya mwambao wa Pwani takriban kila mwisho wa wiki kusambaratisha ngome ya Kiongozi wa chama cha ODM na muungano wa Nasa, Raila Odiga.
Makamu wa Rais amefanikiwa kurusha ndoano na kuwanasa samaki wengi wakubwa kama vile nyangumi na papa.
Hatua ya Ruto haijapokelewa vyema na ODM ambayo sasa wanapanga mkutano wa dharura kujadili ziara za kiongozi huyo katika maeneo hayo na kutafuta suluhu ya kuzuia viongozi zaidi kumuunga mkono katika safari yake ya 2022.
Kamati kuu ya kitaifa ya chama hicho itakutana wiki hii ikiwa na ajenda ya kuziba nyufa zinazosababishwa na ziara za Ruto.
Raila anatarajiwa kuongoza kikao hicho baada ya shughuli nyingi za wiki jana za kujaribu kuwapatanisha viongozi wa Sudan Kusini wanaozozania uongozi.
Kiongozi huyo alirejea Juni 10 kutoka Afrika Kusini ambapo alikutana na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar.
Mkutano huo utaamua jinsi ya kuwaadhibu wanasiasa wa ODM wanaokaidi kanuni za chama. Wanasiasa wanaolengwa kuadhibiwa ni wale ambao wamekuwa wakimlaki na kuongozana na Ruto katika ziara zake za Pwani ambazo zimezidi kwa miezi miwili iliyopita. Kamati ya adhabu itakuwa na kazi kwa sababu idadi ya wanasiasa (wabunge, maseneta na magavana) ambao wanamuunga mkono Ruto ni kubwa.
ODM ina kila sababu kupata tumbo joto kutokana na kampeni za mapema za makamu wa Rais. Miongoni wa wabunge 46 wa ODM katika Bunge la Kitaifa kutoka Pwani, 42 wameapa kumpigia debe Ruto hadi 2022.
Pwani ina magavana sita (mmoja wa Jubilee na waliosalia wakiwa wa ODM. Kwa sasa ni Gavana Hassan Joho pekee ambaye hajamfuata Ruto. Kwa ufupi, magavana watano wameingia katika kambi ya Ruto.
Raila ataambulia chochote?
Swali la kujiuliza sasa ni iwapo Raila ataponea chupuchupu katika mazingara haya na mawimbi ya Ruto katika eneo hili ambalo kwa miaka kadhaa limekuwa ngome yake.
“Kuna sintofahamu kwenye chama chake kwa sasa. Hakuna anayejua kama Raila atawania urais 2022 au la. Anahitaji kujitokeza na kusema kama atakuwa miongoni mwa wale watakaowania kiti hicho au la,” mwanachama mmoja wa Kamati Kuu ya ODM alisema.
Makamu wa Rais amekuwa akitumia nguvu zake na ushawishi wake wote kuwaweka mfukoni wanasiasa wa ODM katika maeneo ya Nyanza, Magharibi mwa Kenya na Pwani huku akijitayarisha kumrithi Uhuru.
Lakini, Ruto anakanusha madai yoyote yanayoonyesha ameanza kampeni. Anasema yeye yuko katika ziara rasmi za kuzindua miradi ya maendeleo na kumwakilisha Rais Uhuru. Lakini, wadadisi wa siasa hawakubaliani naye, wanasema ameanza kampeni za 2022 huku akipeana “zawadi” na ahadi kwa wale anaowalenga wamuunga mkono.
Kuna tofauti kati ya Ruto anayefanya kampeni na Ruto anayetekeleza majukumu ya kiserikali kama vile uzinduzi wa miradi mbalimbali.
Ruto ambaye Wakenya wanamuona sasa katika ziara, ni mtu ambaye yuko kwenye pilikapilika za kampeni rasmi. Lengo la Ruto ni kutayarisha na kuimarisha kampeni zake ili wengine watakapoanza zao miaka mitatu au minne kuanzia sasa, atakuwa amepiga hatua.
Madhara yake
Harakaharaka zake zinaweza kuhujumu ndoto zake kwa sababu 2022 bado ni mbali mno. Wakati wanasiasa wengine watakapokuwa wanaanza kampeni zao, Ruto na wafuasi wake watakuwa wamechoka. Wananchi wengine watakuwa wamebadilisha mawazo yao na kuanza kuegemea upande wa wanasiasa “wapya”.
Ruto alizindua mradi wa Ksh3.2 bilioni katika eneo la Shimoni katika Jimbo la Kwale. Hii ni moja ya miradi mingi ambayo amezindua katika eneo la Pwani. Bila shaka, hii itasaidia kuwavutia wananchi kumpigia kura 2022.
Kwa siku tatu mfululizo, Ruto aliweka kambi Pwani ambapo amemiminiwa sifa na wanasiasa wa upinzani. Vitisho vya Katibu wa ODM, Edwin Sifuna kuwa atawaadhibu wanasiasa hao vimepuuziwa huku wanasiasa wa ODM wakisisitiza kuwa wataendelea kumpigia debe Ruto hadi mwisho.
Tangu Rais Uhuru na Raila kukutana Machi 9 na kuzika tofauti zao, Ruto amefanya mikutano 46 ya hadhara kote nchini. Ruto hufanya mikutano mitatu kwa wiki moja.
Kama mwanafunzi kamili wa Rais mstaafu, Daniel arap Moi, Ruto anazingatia michakato ileile ya kukutana na wananchi kila siku na pia kuwaalika viongozi nyumbani kwake, Eldoret na Nairobi.
Kila wakati anapozindua miradi, Ruto pia hutumia fursa hiyo kukutana na viongozi wa maeneo ambayo miradi hiyo inazinduliwa.
Ziara hizo za Ruto hazijamfurahisha Rais Uhuru ambaye wiki mbili zilizopita alisema Ruto anafaa kuacha “kutangatanga katika vichochoro”.
Duru za kuaminika zinasema kwamba Ruto huwa anaahidi kuwatunza wanaomuunga mkono atakapokuwa rais.
Wabunge wa ODM wajitosa
Baadhi ya wabunge wa chama cha ODM waliomwacha Raila na kumfuata Ruto wanasema makamu wa rais ni mtu ambaye si mchoyo na ameendelea kuwaletea miradi ya maendeleo.
“Ruto sasa haongozi katika orodha ya wanasiasa wanaogombea urais. Yeye ni mgombea wa kipekee ambaye anatuletea suluhisho la matatizo yetu huku tukielekea 2022,” akasema Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa.
Jumwa ambaye sasa anajulikana kwa jina la Mama Radar kwa sababu ya machachari yake anapompigia debe Ruto, alikuwa mfuasi sugu wa Raila. Jumwa ni miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kumfuata Ruto.
Ruto ameleta mawimbi makali katika ngome ya Raila katika eneo la Nyanza. Mnamo Aprili 8, Makamu wa Rais alikutana na wabunge watano kutoka Jimbo la Nyamira na kutangaza kwamba shule katika kanda hii zitafaidika kwa Ksh2.1 bilioni.
Mapema kabla ya mkutano huo, Ruto alikuwa amefanya mkutano na wabunge wote tisa kutoka Jimbo la Kisii na kuwashauri wajitenge na mizozo iliyosababishwa na uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kushirikiana katika miradi ya maendeleo.
Katika nyumba yake mtaa wa kifahari wa Karen, Nairobi, Ruto amekutana na wabunge kutoka eneo la Magharibi. Mkutano huu ulichochea mawazo kwamba huenda Ruto anapanga kushirikiana na kiongozi wa chama cha Ford-Kenya, Moses Wetangula na mwenzake wa ANC, Musalia Mudavadi.
Kwa miaka 15 iliyopita, Raila amekuwa ana wafuasi kutoka Nyanza na Magharibi ambapo alipata asilimia 70 ya kura katika sehemu hizi mbili zenye wapiga kura wengi.
Naibu mwenyekiti wa ODM, Gavana Wycliffe Oparanya wa Jimbo la Kakamega amekutana na Ruto huku kukiwa na fununu kwamba anapania kuwa mgombea mwenza wake.
Kiranja wa Kundi la wachache katika Bunge la kitaifa, Junet Mohamed ameonya kwamba kampeni za mapema zimeng’oa nanga na kuna hatari ya kufungua mianya ya matumizi na uvujaji wa pesa za umma. Huku Ruto akiendelea kujenga ufuasi wake, washiriki wake wa kisiasa wanasema hawajafurahishwa na jinsi vita dhidi ya ufisadi vinavyotekelezwa.
Kiongozi wa walio wengi bungeni, Aden Duale na Seneta wa Jimbo la Nandi, Kiprotich Cherargei wanadai vita hivyo vilivyoanzishwa na Rais Uhuru wiki tatu zilizopita, vinalenga watu walio na uhusiano wa kisiasa na makamu wa Rais.