Samaki Pia Wana Maumbile Tofauti Kama Binadamu- Msukuma

Samaki Pia Wana Maumbile Tofauti Kama Binadamu- Msukuma
Mbunge wa Geita vijijini (CCM), Joseph Musukuma amesema kuwa samaki wako wa aina tofauti Ziwani na wengine wana tabia kama binadamu kwa kile alichodai wana maumbile madogo lakini wana umri mkubwa.

Musukuma ametoa kauli hiyo bungeni leo, wakati akihoji swali la nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu kwa wizara ya mifugo na uvuvi ambapo amesema kuwa suala la kupima kwa rula samaki haliafiki kwa kuwa viumbe hao pia wana maumbile tofauti kama binadamu.

“Dhana ya uvuvi haramu imeenea sana, lakini samaki pia wana maumbile tofauti kama binadamu na mfano ukichukua umri wangu mimi na mheshimiwa Mwalongo tunalingana lakini ukitutazama maumbile tunatofautiana sana, sasa hata samaki wako hivyo, kwahiyo hata samaki wakipimwa kwa rula hawalingani, sheria haijalitazama hilo, Je ni lini sheria itamtazama mvuvi na kumlinda pindi anapokumbana na changamoto hii ya samaki kuwa na maumbile tofauti na umri wake?”, amehoji Musukuma.

Akijibu swali hilo Naibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amekiri kuwa sheria ina mapungufu na itafanyiwa maboresho ili kuhakikisha inawapa ahueni pia wavuvi katika shughuli zao.

Sanjari na hayo Ulega ameongeza kuwa kumekuwa na malalamiko ya kuteketezwa kwa nyavu bila kufanyiwa uchunguzi na wavuvi wengi wamekuwa wakionewa, na wizara itawachukulia hatua watendaji wote wa sekta hiyo wanaotenda kinyume na taratibu.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad