Serikali imesema kuwa, kamati maalumu iliyoundwa inaendelea na zoezi la uhakiki wa kupitia mikataba yote ya wasanii nchini, ili kusaidia wasanii waweze kunufaika na kazi zao kutokana na makubaliano ya kibiashara waliyoingia.
Hayo yamesemwa Bungeni leo Juni 18, 2018, Jijini Dodoma, na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti maalum Bi Martha Mlata aliyetaka kujua ni kwa namna gani serikali inasaidia wasanii kunufaika na kazi zao.
“Sasa hivi tumeunda kamati ambayo inapitia mikataba yote ya wasanii, sasahivi tumefikia hatua nzuri tunaamini kwamba kamati hiyo itakapokamilisha kupitia mikataba yote nchini, tunaamini kabisa kwamba wasanii wataweza kunufaika na kazi zao” amesema Shonza.
Naibu Waziri Shonza ameongeza kuwa serikali imekuwa ikitoa elimu ya mara kwa mara kwa wasanii nchini ili wafahamu umuhimu na namna ya kuhifadhi kazi zao pamoja na kusimamia haki za kisanii ili kuepuka changamoto ya kuingia katika mikataba ambayo haizingatii maslahi yao kama wasanii.
Kwa upande mwingine Naibu Waziri huyo amedai kwamba serikali inafanya mazungumzo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuirudisha Idara ya Chama cha Hakimiliki nchini (COSOTA) katika usimamizi wa Wizara ya Habari, Utamadiuni Sanaa na Michezo ili kuwezesha masuala yote ya wasanii kuwa chini ya mwamvuli mmoja.