Mchezaji wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shaaban Idd Chilunda amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi kuu soka Tanzania Bara (VPL) kwa mwezi Mei.
Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) alasiri ya leo Juni 08, 2018 na kusema Chilunda alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Jacob Massawe wa Ndanda na Edward Shija wa Kagera Sugar katika uchambuzi uliofanywa wiki hii na kamati ya tuzo hizo.
Chilunda aliisaidia Azam FC akifunga mabao 6 kwa mwezi huo, ambapo kati ya mabao hayo matatu 'hat trick' alifunga katika mchezo mmoja.
Kwa mwezi huo Azam ilicheza michezo minne na kupata pointi tisa, baada ya kushinda michezo mitatu na kufungwa mmoja ikibaki katika nafasi yake ya pili na hakuwa na kadi yoyote. Kwa upande wa Shija aliisaidia Kagera Sugar kupata pointi 10, akifunga mabao matatu katika michezo minne iliyocheza timu yake, ikishinda mitatu na kutoka sare mmoja na kupanda kutoka nafasi ya 12 iliyokuwepo mwezi Aprili hadi ya tisa.
Massawe alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha timu yake kuepuka kushuka daraja ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu, akiisaidia kushinda mechi mbili kati ya nne walizocheza na hivyo kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 15 hadi ya 14 katika timu 16 zilizoshiriki ligi hiyo.
Kutokana na ushindi huo, Chilunda atazawadiwa tuzo, fedha taslimu sh. 1,000,000 (milioni moja) pamoja na zawadi mbalimbali kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo.