Wakati vita ya kupambana na madawa ya kulevya ikionekana kufanikiwa kwa kiasi flani hapa nchini, taarifa mpya iliyotua kwenye dawati la gazeti hili ni kwamba, hivi karibuni Watanzania watatu wamepandishwa kizimbani Texas, California nchini Marekani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo haramu.
Akizungumza na UWAZI kwa njia ya simu, Kamishna wa Sheria wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Edwin Kakolaki amewataja Watanzania hao kuwa ni Ally Haji ‘Shikuba’, Iddy Mfuru na Tiko Adam ‘Tikotiko’ ambao kesi yao imeshaanza kusikilizwa nchini humo.
“Katika uendeshwaji wa kesi hiyo tumekuwa tukishirikiana na Marekani kwa kupeana taarifa mbalimbali kwa kila kinachoendelea.
“Taarifa walizotuletea hivi karibuni ni kwamba wameshawapandisha kizimbani na kuwasomea mashitaka yao ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya,” alisema Kakolaki. Alisema watu hao wanashitakiwa kwa makosa ya kusambaza na kujihusisha na biashara hiyo haramu nchini Marekani.
Wakati watuhumiwa hao wakihenyeshwa kortini, hapa nchini mambo yanazidi kuwa moto kufuatia mamlaka ya kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya kuonesha kujizatiti kuhakikisha wafanyabiashara wanaotumia njia za panja kuingiza madawa hayo hawafui dafu.
Akizungumzia hilo, Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka hiyo ya kuzuia madawa ya kulevya nchini, Frederick Kibuta alisema cocaine na heroine hazizalishwi hapa nchini, zinatoka nje ya nchi na kuingizwa kwa njia mbalimbali.
“Kwa upande wetu tunapambana kuhakikisha madawa hayo hayaingii nchini kwa namna yoyote, iwe kupitia mipakani au viwanja vya ndege, tumejizatiti vilivyo,” alisema.
TUJIKUMBUSHE YA AKINA SHKUBA
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, chini ya Hakimu Mkazi, Cyprian Mkehe Aprili 12, 2017 ilikubali ombi la Wizara ya Sheria na Katiba la kuruhusu mtuhumiwa wa kusafirisha madawa ya kulevya, Shkuba na wenzake wawili, Mfuru na Tikotiko, wasafirishwe kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha madawa ya kulevya.
Chanzo: Global Publishers