HII ni habari njema kwa mashabiki wa Simba, ni kwamba leo kipa wa zamani wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ anasaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba.
Dida awali aliwahi kuwa kipa wa Simba, akaondoka na kwenda Yanga na baadaye akakimbilia Afrika Kusini ambapo alijiunga na timu ya Tucks ya nchi hiyo, ambapo taarifa zilisema kuwa hakuwa anapata nafasi ya kutosha ya kucheza.
Hata hivyo, hivi karibuni kipa huyo alitua hapa nchini na taarifa kusema kuwa anajiunga na timu ya Yanga, Championi likamtafuta na kuzungumza naye ambapo aligoma katakata, lakini habari ambazo tumezipata ni kwamba anasaini kuichezea Simba leo.
Chanzo cha ndani cha uhakika kutoka kwenye uongozi wa Simba, kimesema kuwa Dida atasaini mkataba wa miaka miwili leo ikiwa ni siku moja tu baada ya Meddie Kagere na Pascal Wawa kutua kwenye kikosi hicho cha Msimbazi.
“Taarifa ni kwamba saa chache zijazo au kesho asubuhi Dida atasaini mkataba wa kuitumikia Simba, bado haijafahamika ni miaka mingapi kwa kuwa inafanywa siri lakini haiwezi kuwa chini ya miwili kwa kuwa mwenyewe alitaka hivyo.
‘’Analetwa ili kumpa upinzani Aishi Manula na inaonekana kuwa Said Mohammed ‘Nduda’ atapelekwa kwa mkopo kwa msimu ujao kwa kuwa Simba wanaamini kuwa ni kipa mzuri lakini majeraha ndiyo yalimsumbua msimu uliopita,” kilisema chanzo hicho ambacho kipa karibu na benchi la ufundi la timu hiyo.