Mabingwa wa soka nchini klabu ya Simba imekamilisha usajili wa mshambuliaji Meddie Kagere kutoka klabu ya Gor Mahia ya Kenya. Kagere ambaye ni raia wa Rwanda amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo.
Dau la usajili wa mshambuliaji huyo ambaye amewika na klabu ya Gor Mahia kweney mashindano mbalimbali msimu uliopita ikiwemo michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika limetajwa kuwa ni dola 60,000 zaidi ya milioni shilingi 120.
Mbali na dau hilo la usajili ambalo linatua kwa klabu yake ya Gor Mahia, Kagere amesaini kulipwa mshahara wa dola 5,500 sawa na shilingi milioni 11 kwa mwezi pamoja na kupewa gari na nyumba ya kuishi yenye kila kitu.
Kagere ni miongoni mwa washambuliaji ambao walijizolea umaarufu kweney ukanda huu wa Africa Mashariki na kati baada ya kufunga mabao 3 kwenye michuano ya SportsPesa Super Cup nchini Kenya na kuisaidia timu yake ya Gor Mahia kuibuka mabingwa wa michuano hiyo.
Mnyarwanda huyo anaungana na nahodha wa timu yake ya taifa Haruna Niyonzima ambaye naye atakuwepo Simba kwa msimu wa pili sasa baada ya kusajili msimu uliopita akitokea Yanga. Hata hivyo Gor Mahia imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Vipers ya Uganda Erisa Ssekisambu kwaajili ya kuziba nafasi ya Kagere.