PENYE siri iliyofichwa na wengi husubiri wakati na sababu ili ifichuke, ndiyo maana Waswahili husema ‘hakuna siri ya watu wawili,’ Ijumaa kupitia vyanzo vyake limebaini kuwa ajali aliyopata hivi karibuni baunsa wa Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Mondi’ aitwaye Mwarabu Fighter imezua mambo mazito.
Ingekuwa bora kama ingezua mazito tu lakini habari zinasema imewafikisha pabaya, mawashiba hao wanaofanya kazi kampuni moja ya Wasafi Classic Baby ‘WCB’ ambapo bosi wa Mwarabu ni Mondi.
Ukichungulia kapu la mambo mazito limejaa tuhuma kibao mara “Mondi hakumpa pole Mwarabu alipopata ajali. Ametelekezwa kimatibabu na baunsa huyo alishalikoroga WCB zamani na kufungashiwa virago.” Hayo ni kwa uchache mengine yanakuja.
TUANZE NA MONDI KUTOTOA POLE
Ijumaa halipitwi na mambo ya udaku kamwe; paap mara tu baada ya Mwarabu kupata ajali ya kuanguka na bodaboda aliyopata Juni 22, mwaka huu, eneo la Mbezi Afrikana jijini Dar, zikaanza tetesi kwamba baunsa huyo hakupewa pole na bosi wake.
“Nakuambia hakumpa pole, alichokifanya aliposti tu kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram kutokea Marekani alipokwenda kufanya shoo habari kuwa Mwarabu Fighter kapata ajali,” chanzo kililidokeza Ijumaa.
Pengine kwa kupima uzito wa ishu wakuu wa dawati la habari nyeti wa Global Publishers waliona kutojuliwa hali ni kitu kidogo, wakaiweka kando tetesi hiyo, lakini upepo wa mambo mazito haukutulia baina ya watu hao.
Siku tatu baadaye ikaja habari kwamba Diamond ambaye yuko nje ya nchi mbali na kutompa pole mlinzi wake hakujishughulisha chochote kumuuguza.
“Ukitaka uhakika nenda nyumbani kwa Mwarabu kamuulize, si Diamond wala WCB waliomhudumia, anahangaika mwenyewe na familia yake, inasikitisha sana,” chanzo chetu kilisema.
IJUMAA LASHAURIWA
Baada ya kupewa ushauri huo wa kwenda kumuona Mwarabu Fighter, Ijumaa liliona kuwa hiyo ni kazi ndogo, lakini muhimu kwanza kuperuzi na kujua zaidi tuhuma hizo kwamba inawezekanaje mtu asipewe pole na kisha kutelekezwa na bosi wake bila kuwepo kwa ishu inayosababisha hayo yatokee?
Timu ya uchunguzi ilipoingia kazini kwa saa chache tu ikabaini mambo mengine mazito ambapo yalikusanywa tayari kwenda kuyapatia majibu kwa Mwarabu Fighter na upande wa Mondi na WCB.
HUYU HAPA MWARABU
Alipoulizwa na Ijumaa lililomtembelea nyumbani kwake Mbezi Afrikana juzi (Jumanne) kuhusu habari za kutelekezwa Mwarabu alisema:
“Labda linaweza kuwa neno kali sana kusema nimetelekezwa, lakini ukweli ni kwamba sijapata huduma zozote kutoka kwa Diamond au WCB, pengine wanajipanga kunisaidia siwezi kujua.
“Kwa sasa nahangaikia afya yangu mwenyewe; nashukuru naendelea vizuri nina imani nitapona,” alisema Mwarabu huku akikiri pia kwamba hakupokea SMS wala simu kutoka kwa bosi wake iliyotaka kumjulia hali zaidi ya kuona hiyo posti ya Instagram aliyoweka Mondi.
BADO ATAMLINDA MONDI
“Kimsingi watu walikuwa hawajui, mimi nilisimamishwa kazi muda mrefu, tangu mwezi wa pili mwaka huu, niliambiwa tu nibaki nyumbani mpaka nitakapoitwa.
“Basi muda wote huyo nimekuwa nikifanya mazoezi na kufundisha vijana mambo ya ngumi, kwa hiyo ukiniuliza kuhusu kumlinda Diamond nitakuambia kwa sasa simlindi pengine yatakayofuata baadaye yatajulikana huko,” alisema Mwarabu Fighter.
Habari kutoka chanzo chetu zinadai kuwa baunsa huyo wa Mondi aliyefanya naye kazi kwa zaidi ya miaka mitano mkataba wake na maslahi yake yamekuwa na chengachenga.
“Hataki kusema lakini Mwarabu Fighter mkataba wake ulikuwa umemalizika na alikuwa akihangaika mara kadhaa kuwaomba wamuongezee mshahara lakini wamekuwa wakimzungusha,” chanzo kilieleza hivyo maelezo ambayo Mwarabu hakutaka kuyatolea ufafanuzi.
“Mambo ya mkataba na kazi zangu WCB yatabaki kuwa siri, kwa sasa afya yangu ni muhimu kuliko kitu kingine,” Mwarabu alisema na kuongeza kuwa muda ukifika wa kuweka wazi mambo yote atafanya hivyo.
TUCHIMBE MWARABU KUPEWA LIKIZO
Jambo linalofikirisha zaidi lilikuwa ni pale Mwarabu aliposema kwamba aliambiwa abaki nyumbani mpaka atakapoitwa, huku sababu ikipotelea hewani bila kuwekwa wazi na mwenyewe au mabosi wa WCB, jambo ambalo Ijumaa iliona haliwezi kubaki bila kupatiwa majibu.
Uchunguzi uliofanywa ukihusisha vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii ulibaini kuwa Mondi na baunsa huyo uelewano wao uliyumaba miezi michache iliyopita.
Yapo madai kwamba Mondi na Mwarabu walijikuta wakikosana kikazi kwa kile kinachotajwa kuwa ni kutoaminiana kwa baadhi ya wana familia ya WCB juu ya mambo ya ‘totoz.’
Itakumbukwa kwamba Mwarabu aliwahi kuhusishwa kutoka kimapenzi na demu wa Harmonize aitwaye Sarah jambo ambalo lilizua mtikisiko na kumuweka baunsa huyo kwenye ramani mbaya kuwa ‘HAAMINIKI’.
Hata hivyo tuhuma hizo ambazo ziliandikwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari zilikanushwa na zinakanushwa hadi sasa na Mwarabu kuwa hawezi kufanya hivyo na kwamba kilichotokea ulikuwa ni mpango wa wabaya wake kumchafulia jina.
WCB, MONDI WANASEMAJE?
Ijumaa liliona kwamba baada ya kuwepo kwa tuhuma nyingi juu ya Mondi na WCB kwa ujumla liliona ipo haja ya kuwatafuta wahusika ili kujua upande wa pili wa shilingi, kwa bahati mbaya hawakuweza kupatikana,
Mondi simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikana huku Said Fella, Babu Tale ambao ni miongoni mwa mameneja simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa na kwamba juhudi za kuwatafuta zinaendelea.
GPL