Spika wa Bunge, Job Ndugai amelazimika kutoa ya moyoni baada ya kuwepo na taarifa za kususia mazishi ya Mbunge wa Buyungu, Mwl. Kasuku Bilago ambapo amesema kuwa kamwe asingeweza kwenda kwenye uwanja ulioandaliwa na vyama vya siasa kujadili Mbunge gani atafuata kuchukua jimbo hilo.
Akitoa ufafanuzi huo leo bungenii Spika Ndugai amesema kwamba asingeweza kufanya biashara hiyo ya kuanza kunadi siasa msibani kwani ni jambo ambalo hajawahi kufanya na hataweza kufanya kwani hata maspika waliopita hawakuweza kushiriki mazishi kwenye viwanja vya siasa.
Ndugai amesema utaratibu wa siku zote wa Bunge, marehemu huwa anapelekwa kwa familia na anaagwa kwa familia kisha kupelekwa makaburini kama utaratibu unakuwa umekamilika watu wote humaliza msiba eneo hilo lakini utamaduni wa kupelekwa viwanjani hata kama angekuwa kiongozi wa Chama gani Spika asingeweza kwenda viwanjani.
Mbali na hayo, amesema kuwa kutokana na utaratibu wa Watanzania watu huwa 'hatugombei msiba' ndiyo maana walikabidhi mwili wa marehemu Bilago kwa familia kwa kufuata utaratibu kwa kuwa Bunge kama Taasisi lilipanga kumaliza msiba Mei 30.
Hata hivyo Spika Ndugai amefafanua kuwa familia ndiyo yenye mamlaka na marehemu na wao ndiyo wenye maamuzi ya kubadilisha ratiba pindi wanapokuwa wanahitaji.
Pamoja na hayo Ndugai amemtaka Mh. Selasini pamoja na viongozi wengine (hawajatajwa majina) wanaoshiriki vikao na kupata maamuzi ya pamoja kisha wanaenda kutoa taarifa tofauti waache kwani ni jambo lisilo na maana hata kidogo.