SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amemuwakia Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na kueleza masikitiko yake kufuatia kitendo cha maofisa wa wizara hiyo kuingia eneo la Bunge (mgahawa wa bunge) na kupima samaki kwa rula kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wachanga na wamevuliwa kinyume cha sheria.
Ndugai ameyasema hayo leo Jumatano, Juni 20, 2018, Bungeni jijini Dodoma kufuatia Waziri Mpina kuliomba radhi Bunge baada ya maofisa wa wizara yake kuingia katika mgahawa wa bunge na kupima urefu wa samaki waliopikwa kisha kumpiga faini mmiliki wa mgahawa huo kiasi cha Tsh. 300,000 kwa madai ya kukutwa na kilo mbili za samaki wachanga (chini ya sentimita 25) waliovauliwa kinyume cha sheria.
“Tunamshukuru Waziri kwa maelezo aliyoyatoa, lakini tunasikitishwa na kilichotokea, mabunge mengine ya nje wakisikia kuna waziri hapa nchini amefanya kilichofanyika, itakuwa ni dharau sana, hata panapokuwa na kosa limefanyika eneo la bunge, RPC anapaswa kunijulisha.
“Watu wananunua samaki kwa kilo na si kwa futi, halafu samaki mwenyewe kapikwa, kishakuwa ni kitoweo, hii sheria ya kupima kitoweo inabidi tuisome vizuri, hivi Watanzania wawe wanafunga milango ndiyo wale samaki?
“Wapimaji wenyewe wa wizara wanapima chakula cha waheshimiwa wakati mikono yao hawajavaa hata gloves, tena wamearika na waandishi wa habari, huu ulikuwa kama mpango maalum wa kuliweka bunge katika hali flani,” alisema Ndugai.