Katika hali isiyotarajiwa, kocha mkuu wa Simba, Pierre Lechantre ametoweka klabuni hapo huku ikiwa haijaeleweka mara moja kama amerejea jijini Dar es Salaam ama kwao Ufaransa.
Inasemekana kwamba Lechantre amekasirishwa na kitendo cha mabosi wa timu hiyo kumchunia kumpa mkataba mpya huku kukiwa na ukosoaji mkubwa wa namna timu ya Simba inavyocheza kwa sasa hivyo kuamua kuondoka.
Habari za kutoka ndani ya Simba zimebainisha kuwa kocha msaidizi, Masoudi Djuma ndiye anakaimu nafasi hiyo kwa sasa na ndiye atakuwepo kwenye benchi wakati Simba ikicheza na Kakamega Homeboys katika nusu fainali ya SportPesa, leo Alhamisi.
Viongozi wa Simba wameshindwa kuwa na majibu wa uhakika juu ya Lechantre huku wakidai kuwa watatoa taarifa kamili mara baada ya mechi hiyo ya nusu fainali.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tulily ambaye yuko na timu hiyo mjini hapa alisema watatoa taarifa kamili baada ya mchezo huo wa nusu fainali.
Lechantre alijiunga na Simba mapema mwaka huu na kufanikiwa kuipa taji la Ligi Kuu Bara walilokuwa wamelikosa kwa misimu mitano mfululizo.