Tanzania Inaongoza Kwa Uchumi Kusini Mwa Jangwa La Sahara-majaliwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema taarifa ya Kongamano la Uchumi la Dunia la mwaka 2018 inaonesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na uchumi jumuishi miongoni mwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.


Amesema hali hiyo, imetokana na Tanzania kufungua fursa za ujasiriamali ambapo kuna zaidi ya biashara milioni tatu zinazokuwepo kila mwaka, lengo la nchi ni kuhakikisha kuwa uchumi unakua na unamgusa kila Mtanzania hususan mwananchi wa kawaida.


Waziri Mkuu ameyasena hayo leo (Jumatatu, Juni 18, 2018) wakati akifunguaKongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa LAPF, jijini dodoma.


“Pia, huduma za fedha jumuishi ni kigezo ambacho kimeiweka Tanzania mahala pazuri kwenye uchumi jumuishi ambapo zaidi ya Watanzania milioni 30 wamekuwa wakifanya miamala mbalimbali ya fedha kupitia simu za mkononi na hivyo kuongeza huduma za fedha kufikia asilimia 65,” amesema.


Amesema huduma za msingi za kijamii kama vile elimu, afya na kupungua kwa rushwa katika utoaji huduma za umma pamoja namtandao wa miundombinu ya barabara ambayo huwezesha wananchi wengi kujishughulisha na shughuli za kiuchumi ni kigezo kingine kilichozingatiwa katika kuipatia Tanzania nafasi hiyo.


Waziri Mkuu ameongeza kwamba Serikali inaamini kuwa uchumi wa viwanda ukiimarika uchumi utakuwa kwa kasi kubwa na matokeo yake yataonekana wazi kwa kupanua wigo wa ajira, soko la huduma na shughuli nyingine za kiuchumi.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema suala la uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ni moja ya ajenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo amezitaka sekta zote zihakikishe zinatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa viwanda.


Pia amesema suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi lazima liende sambamba na uwezeshaji vijana kujiajiri kama inavyoelekeza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015. “Ilani inatambua kwamba kuwawezesha wananchi kiuchumi ni hatua ya msingi katika kujenga Taifa lililoimarika kiuchumi na lenye lengo la kujitegemea,”.


Aidha, Ilani pia, inasisitiza kuhusu umuhimu wa kuhamasisha ushiriki wa Sekta binafsi katika kuwezesha wananchi kiuchumi, hivyo ni muhimu kukamilisha taarifa ya uwezeshaji kutoka kwa wadau wa sekta binafsi, ili Serikali iweze kuona mchango wa sekta binafsi katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.


Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa malengo hayo ya uwezeshaji wananchi katika maeneo ya fursa za mafunzo ya ujasiriamali na mikopo ya masharti nafuu ni muhimu sana katika kupambana na umaskini wa kipato.


Amesema kwa kutambua umuhimu wa ajenda ya uchumi wa viwanda, ndiyo maana makongamano ya uwezeshaji yamekuwa yakiweka mkazo kwenye masuala ya viwanda. Hali hiyo pia, inajidhihirisha katika kaulimbiu ya Kongamano la Tatu ambayo ni: “Viwanda: Nguzo ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi”.


Hivyo Waziri Mkuu ameongeza kwa kusema, “tuendelee kuhimiza kuhusu kutekeleza uchumi wa viwanda kwa lengo la kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi na kuhakikisha kuwa tunafikia lengo la kuwa na  uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,”.


Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba, Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Bw. Suleiman Jafo.


Wengine ni Wakuu wa Mikoa mbalimbali, Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Wilaya ya Mkoa wa Dodoma, Makatibu Tawala wa Mikoa, Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,Wakurugenzi wa Halmashauri za Mamlaka za Serikali za Mitaa,


Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’ Issa, wadhamini wa Kongamano hilo na Wawakilishi kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta binafsi.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad