Wamiliki wengi wa blogu katika mitandao ya kijamii nchini wamesema “kwaheri ya kuonana”.
Wamewaaga watumiaji wa blogu hizo ambao walizoea kupata taarifa muhimu za Serikali na matukio mengine ya kijamii kwenye kurasa zao za mitandao ya intaneti.
Sasa hawawezi tena kutuma taarifa hizo kwa kuwa kwanza watatakiwa kulipa Sh100,000, halafu ada ya Sh1 milioni kwa ajili ya kupata leseni na pia uwezekano wa kudhibitiwa baada ya kusajiliwa.“Gharama kubwa za usajili wa leseni zimetushinda. Tunasitisha huduma kwa muda usiojulikana,” alisema mmiliki wa blogu ya Innowisetz, Innocent Shayo kupitia mtandao.
Baadaye akizungumza na Mwananchi kwa simu, Shayo alisema gharama za kupata leseni ambayo ni Sh1 milioni ni kubwa hasa kwa blogu ambazo zimeanzishwa hivi karibuni.
“Serikali ipunguze ili ziweze kulipika kwa urahisi,” alisema.
Shayo alitumia ukurasa wake kuwaaga wasomaji wake akisema hakupenda kusitisha huduma, lakini ameamua kutii agizo la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Shayo ni mmoja wa wamiliki kadhaa wa blogu waliotuma taarifa kwenye mitandao ya kijamii wakisema wanasitisha huduma kwa sababu wameshindwa kulipa gharama za usajili wa leseni. TCRA iliagiza kuwa ifikapo Juni 15 (yaani jana) vyombo vya habari vya maudhui ya mtandao ambavyo havijapata leseni havitaruhusiwa kuweka taarifa au habari zozote kwenye akaunti au kurasa zao. Sharti la usajili wa majukwaa hayo ya mitandaoni ni kwa mujibu wa Kanuni za Maudhui ya Kimtandao zinazolenga kuratibu na kudhibiti matumizi sahihi ya mitandao. Kwa mujibu wa kanuni ya 4 na 14, watu wanaotoa huduma za blogu, majukwaa ya mtandaoni wanatakiwa kujisajiliwa na chombo hicho.
Katika awamu ya kwanza Mei 25, mamlaka hiyo ilitoa leseni 45 kati ya 262 kwa watoa huduma hizo.
Umoja wa Wamiliki wa Blogu Tanzania (TBN) una wanachama 130, lakini waliosajiliwa ni watano.
Mtandao maarufu wa Jamii Forums ulikuwa wa kwanza kuwaaga wasomaji wao kwa kuwaomba radhi kwa usumbufu. “Kutokana na notisi iliyotolewa na TCRA Juni 2018 inayotutaka kusitisha utoaji wa huduma mara moja tunalazimika kutii agizo na tunasitisha,” ilisema taarifa ya mtandao huo.
Mmiliki wa blogu ya Darmpya.com, John Marwa aliungana na wenzake kuwaaga wasomaji, akisema kilichowashinda ni gharama za leseni.
“Tunasitisha huduma ili kuepuka kukwaruzana na TCRA. Masharti yaliyopo kwa sasa hatuwezi kuyatimiza,” alisema. Marwa alisema wataendelea kuiomba Serikali kufikiria upya gharama za kupata leseni ambazo alidai kuwa wengi hawawezi kuzimudu.
Mitandao mingine iliyowaaga wasomaji wake jana kupitia kurasa zao ni pamoja na Blogu ya Habari, mtandao wa Makonda Media na Bongo News.
Hata hivyo muda mfupi baada ya TCRA kuanza utekelezaji wa kanuni za maudhui, wamiliki wa blogu na mitandao ya habari wamenza kutofautiana.
Tofauti hiyo imekuja baada ya baadhi kujisajili na wengine kupinga kwa madai kuwa kanuni zilizopo zinaminya uhuru wa habari.
Mkurugenzi wa Jamii Media inayomiliki mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo alidai kanuni zinalenga kukandamiza uhuru wa utoaji na upataji wa taarifa.
“Watu wanaweza kuona hili jambo ni la mchezo. Kwa kanuni hizi, kwenda kusajili ni kujitia kwenye kitanzi. Tatizo jingine ni kwamba Watanzania hatuna uelewa wa sheria,” alisema.
Melo alisema yapo mambo mengi kwenye kanuni hizo ambayo yanatishia haki ya kupata habari, akitoa mfano wa maelekezo ya kuweka wazi chanzo cha taarifa iliyotolewa.
“Hii ni zaidi ya kusajili na kupata leseni na wapo wanaofikiri inamhusu mtu au blogu fulani, hapana. Hili ni la kila mtu anayetumia simu au kompyuta,” alisema. Wakati huohuo, TCRA imeongeza muda wa usajili wa watoa huduma za maudhui mitandaoni hadi Juni 30, mwaka huu.
Awali, siku ya mwisho ya kujisajili ilikuwa Juni 15. Taarifa iliyotolewa jana jioni na mkurugenzi mkuu wa TCRA, James Kilaba ilisema wale ambao hawajajisajili wanatakiwa kufanya hivyo kabla ya Juni 30.