TFF Yafungua Dirisha la Usajili Kivingine

TFF Yafungua Dirisha la Usajili Kivingine
WAKATI klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zikiwa zimeshaanza usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa mwaka 2018/19, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefungua rasmi dirisha la usajili huku awamu hii likija na mfumo tofauti ukilinganisha na ilivyokuwa mwanzo.

Usajili wa sasa utakuwa tofauti na ullivyozoeleka miaka ya nyuma ambapo msimu ujao watatumia mfumo mpya ujulikanao kwa jina la TFF FIFA CONNECT.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, alisema mfumo huu utafafanuliwa zaidi katika semina ambazo zitaendeshwa kwa kuwahusisha viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
Ndimbo alisema kuwa semina hizo zitaanza mapema kabla ya kuanza kutumika ili kutoa uelewa sahihi wa namna unavyopaswa kutumika kwa timu zote husika.
"Semina ya kwanza itaanza kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ambayo itafanyika Jumatatu ya Juni 25 mwaka huu, halafu  itaendelea tena kesho yake itakayokuwa Jumanne kwa zile timu za Ligi Daraja la Kwanza na Jumatano utahusisha klabu za ligi Daraja la Pili," alisema Ndimbo.
Aliongeza kuwa, kutokana na mabadiliko ya mfumo huo wa usajili, TFF imeweka muda wa wiki moja kwa ajili ya kuweka mapingamizi endapo yatakuwepo ambapo klabu zinatawasilisha kupitia kamati maalum itakayosimamia suala la usajili huo.
"Tunawaomba viongozi wa klabu zote kuzingatia muda wa mafunzo ya juu ya mfumo huo mpya ili kuepusha matatizo ambayo yanaweza yakajitokeza baadaye," alisisitiza Ndimbo.
Aliweka wazi kuwa dirisha la usajili tayari lilishafunguliwa tangu Juni 15 na litafungwa ifikapo Julai 26 mwaka huu.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad