Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata na kutaifisha boksi 41 za mvinyo na pombe kali zilizokutwa katika duka la jumla jijini Dodoma zikiwa hazina Stempu za Kodi.
Boksi hizo zenye thamani ya shilingi milioni tatu ambazo ni mali ya Anthony George, zimekamatwa na kutaifishwa leo wakati Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere akikagua matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) Jijini hapa kwenye maduka na vituo mbalimbali vya mafuta.
Akizungumza mara baada ya kutaifisha boksi hizo, Kichere amesema kuwa, ni wajibu wa muuzaji kuhakikisha kwamba, vinjwaji vinavyostahili kuwekewa Stempu za Kodi vinakuwa na stempu hizo ili kuisaidia Mamlaka kutoza kodi stahiki.
"Inatakiwa Stempu za Kodi ziwekwe kwenye mzigo kabla mzigo huo haujanunuliwa na wauzaji wa rejareja. Hii itaisaidia TRA kukusanya kodi halali na hatimaye kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali," alisema Kichere.
Mvinyo na pombe kali zilizokamatwa na kutaifishwa ni pamoja na boksi 27 za Robertson, boksi 7 za Jameson, boksi 5 za Drostdy Hof na boksi 2 za Alko Dompo.
Wakati huo huo, Kamishna Mkuu Kichere amemkamata Dereva wa Bodaboda Issa Athumani na kumtoza faini ya shilingi 30,000 baada ya kununua mafuta ya bodaboda hiyo bila kudai wala kuchukua Risiti ya Kielektroniki ya EFD.
Kichere ameeleza kuwa, wananchi ambao hawadai risiti wanatakiwa kutozwa faini ya shilingi 30,000 hadi 1,500,00 au kuhukumiwa kifungo kisichozidi miezi sita kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015.
"Kuna watu ambao hawadai risiti na kuna mwingine nimemkamata leo ambaye nimemtoza faini ya shilingi 30,000 ili iwe fundisho kwa watu wote wanaonunua bidhaa na huduma mbalimbali bila kudai wala kuchukua risiti", aliongeza Kichere.
Aidha, Kamishna Mkuu Kichere ametoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kutoa risiti kila wanapofanya mauzo na wananchi kuhakikisha wanadai risiti kila wanapofanya manunuzi mbalimbali.
"Natoa wito kwa wafanyabiashara wote waendelee kutoa risti lakini pia wanunuaji wadai na kuchukua risiti. Tunataka kujenga utamaduni wa kutoa na kudai risiti ili tuweze kukusanya kodi stahiki," alisema Kichere.
Naye, Mfanyabiashara wa mafuta jijini hapa Faustine Mwakalinga amemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA kwa kutembelea kituo chake cha mafuta na kusema kuwa, zoezi hilo analolifanya litaongeza mapato ya Serikali kwasababu linajenga ukaribu na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.
"Namshukuru sana Kamishna Mkuu wa TRA kwa kutembelea kituo changu cha mafuta na nimefurahishwa sana na jinsi anavyofanya kazi yake ukizingatia leo ni sikukuu. Ukaguzi huu anaoufanya Kamishna Mkuu, utasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili sisi wafanyabiashara," alifafanua Mwakalinga.
Kamishna Mkuu Kichere ametembelea jumla ya Vituo vya Mafuta vinane na maduka 15 ikiwa ni moja ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni Dodoma hivi karibuni.