Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amefunguka na kuwataka Wabunge wenzake bila ya kujali itikadi ya vyama vyao kutoshiriki kwenye hafla ya kupokea na kukabidhi taarifa za kamati maalum za kuchunguza na kushauri sekta ya Uvuvi wa bahari kuu na Gesi asilia iliyopangwa kufanyika kesho.
Lissu ametoa kauli hiyo jana mchana kupitia ukurasa wake wa kijamii mara baada ya Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuutarifu umma kuwa Juni 2, 2018 Spika wa Bunge Job Ndugai atapokea ripoti hizo ambazo zimepangwa kufanyikia katika viwanja vya Bunge mbele ya lango kuu la kuingilia.
Kutokana na hilo, Lissu amedai kitendo hicho ni kinyume na zinaharibu taratibu za kisheria kwa kuwa taarifa za uchunguzi za Bunge huwa zinawasilishwa bungeni tena mbele ya wabunge wote na kujadiliwa endapo itahitajika kabla ya kukabidhiwa serikalini.
"Nawaomba Wabunge wasikubali kushiriki katika maziko haya ya mamlaka ya kikatiba na kikanuni ya Bunge. Wadai taarifa hizi ziwasilishwe kwanza bungeni na kujadiliwa na wabunge, kama Spika Ndugai na watu wake wasipokubali kufanya hivyo, basi nawashauri wabunge wote wasusie hafla hiyo", amesema Lissu.
Pamoja na hayo, Lissu ameendelea kwa kusema "wabunge watakaoshiriki hafla wajue, au waambiwe, kwamba wanashiriki kwa ushiriki au uwepo wao katika mazishi ya mamlaka ya kikatiba ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri serikali kwa kupitia majadiliano bungeni.
"Kwa utaratibu huu, Bunge halitajadili, na watanzania hawataona wala kusikia tena taarifa za kamati za uchunguzi za Bunge kama zile za Richmond wa Bunge la Spika Sitta na Operesheni Tokomeza na Tegeta Escrow wakati wa Bunge la Spika Anna Makinda".
Kwa upande mwingine, Lissu amesema hakuna kanuni ya Bunge inayoruhusu Kamati yoyote ya Bunge kupeleka taarifa yake serikalini moja kwa moja, bila kupitia bungeni na kujadiliwa na wabunge.