Tuzo za Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa mwaka 2017/18 zinatarajiwa kutolewa kesho Jumamosi Juni 23,2018 kwenye ukumbi wa Mlimani City na mdhamini mkuu wa ligi hiyo baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika tangu Juni 20 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Afisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura kinachofuata ni kutangazwa kwa washindi walioshinda katika vinyang'anyiro mbalimbali vilivyokuwa vinagombewa na washiriki hao.
"Zoezi la upigaji kura lilihusisha Makocha wa Ligi kuu, Manahodha wa Timu za Ligi Kuu pamoja na wahariri wa habari za Michezo", amesema Ndimbo.
Kwenye Tuzo hizo timu ya Simba SC ambayo ndio mabingwa wapya wa ligi kuu wamefanikiwa kubakisha majina matatu ya wachezaji kati ya 15 waliokuwa wanawania Tuzo ya mchezaji bora ambao ni Emmanuel Okwi, John Bocco na Erasto Nyoni.