Meli tatu zimeegeshwa nchini Hispania, zikiwa na mamia ya wahamiaji waliookolewa majini wiki iliyopita wakitokea nchini Libya.
Serikali ya Uhispania imekubali kuwachukua, baada ya Italia na Malta kukataa meli hizo zilizowaokoa wahamiaji hao kuegesha katika bandari.
Shirika la msalaba mwekundu limezitaka nchi za jumuiya ya Ulaya, kuiga mfano wa Uhispania kuonyesha mshikamano katika suala la wahamiaji.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Valencia, Mratibu wa shirika la madaktari wasio na mipaka MSF Aloys Vimard, watu waliopo ndani ya meli hizo wamelazimika kusubiria zaidi ya wiki moja,wakati wanasiasa wakijadiliana hatima yao.
"Jambo ambalo hatuhitaji kulisahahu ni maisha ya watu,ambayo serikali za Ulaya zinayapuuza. Watu hawapaswi kuchukuliwa kama mizigo inayotarajiwa kushushwa mahala. Kila mmoja,yeyote ambaye amekumbwa na hali isiyo ya kawaida baharini ni lazima apewe haki sawa," amesema.
"Hatujui ni nini cha tofauti kibinadamu kilichopo kwa binadamu waliomo ndani ya Aquarius, kwa nini wasiruhusiwe kufika kwenye bandari salama kwa wakati. Wakati ni jambo la usalama kwa watu hawa kuletwa sehemu salama,lakini mjadala wa wanaiasa kujadili maisha yao umechukua juma zima hadi sasa."
Naye Naibu mkurugenzi wa kitengo cha dharura cha Jorge Suarez amesema kuwa wahamiaji wengi waliomo ndani ya meli hawana matatizo makubwa kiafya.