DAR Ukimuaga mtu kwamba unasafiri kwenda Zanzibar, zawadi atakayokuagiza umletee ni ubuyu. Hii inaonesha ni jinsi gani watu wanavyoupenda ubuyu!
Ubuyu wa motomoto kutoka mezani kwetu leo ni wa staa wa Bongo Muvi, Kajala Masanja ‘Kay’. Ubuyu huo unamung’unywa kwamba, hivi karibuni anataka kufunga ndoa na kigogo mmoja mwenye ‘mpunga’ mrefu, ishu hiyo imeanikwa.
Chanzo cha karibu cha staa huyo kilianza kutiririka kuwa, Kajala hivi sasa amebadili kabisa mfumo wa maisha, tofauti na alivyokuwa mwanzo.
Ilisemekana kwamba, siku hizi akishaenda kurekodi kipindi chake cha Biko, anarejea nyumbani na kujifungia muda wote.
MSIKIE MTOA UBUYU
“Kajala siku hizi kumuona ni shughuli kwa sababu muda si mrefu anaolewa na kigogo mmoja ambaye amembadilisha maisha yake.
“Ndiyo maana siku hizi huwezi kumkuta akijichanganya hata kidogo kama ilivyokuwa huko nyuma,” alisema mpashaji huyo.
Msambaza ubuyu wetu huyo alizidi kufunguka kwamba, japokuwa staa huyo nyuma alikuwa amefunga ndoa na baadaye wakapata matatizo.
“Sasa hivi huyo kigogo anayemuoa anadai ndiye mtu anayeweza kuishi naye muda mrefu. Hata hivyo, ndoa yao hiyo bado imefanywa kuwa siri,” alisema mtoa ubuyu huyo.
KAJALA AFUNGUKA
Baada ya Ijumaa Wikienda kumwagiwa ubuyu huo, kama kawaida yake lilimtafuta Kajala ili aweke kila kitu wazi ambapo mara ya kwanza alipoulizwa kuhusu hilo alikuwa akikwepa na kumwambia mwandishi kuwa hapendelei kabisa hiyo habari kuwekwa wazi.
Mazungumzo kati ya Ijumaa Wikienda na Kajala ilikuwa kama ifuatavyo;
Ijumaa Wikienda: Vipi Kajala, naona uko bize na maandalizi ya ndoa…
Kajala: Ndoa gani au unanichuria?
Ijumaa Wikienda: Kuna ubuyu kwamba kuna kigogo mmoja anataka kukuoa na anakupa maisha (kila kitu)?
Kajala: Kwa nini mnapenda kusikiliza maneno ya waongeaji? Kama kuna mtu anataka kunioa si mtaniona ndani ya shela tu?
Ijumaa Wikienda: Kwa sababu tulijua ndoa yako ya kwanza haijavunjika, hivyo tulishangaa iweje uolewe?
Kajala: Sidhani kama kuna ndoa ilishavunjika, lakini kama kuna ndoa mtaiona tu, sioni kama kuna faida kuilezea sasa.
Ijumaa Wikienda: Lakini sasa unasemaje, hiyo ndoa ipo au haipo?
Kajala: Hilo ni jambo jema, kama lipo nitaliweka wazi siku si nyingi.