Mikakati ya serikali kudhibiti utoroshwaji wa madini ya tanzanite imefanikisha mapato ya madini hayo kuongezeka, ikielezwa kuwa mapato ya miezi mitatu (Januari hadi Machi, mwaka huu) yamezidi ya miaka mitatu iliyopita.
Imeelezwa kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya uamuzi wa Rais John Magufuli alioutoa Septemba 20, mwaka jana, wa kujengwa ukuta kuzunguka eneo la migodi ya tanzanite iliyoko Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara.
Agizo hilo la Rais lilitekelezwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kujenga ukuta huo kuanzia Novemba Mosi hadi Februari 15, mwaka huu.
Akiwasilisha hotuba bungeni jijini Dodoma jana kuhusu makadirio ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Wizara ya Madini, Angellah Kairuki, alisema mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na udhibiti wa tanzanite.
Alisema katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, wizara yake imekusanya mrabaha wa Sh. milioni 714.6.
Kairuki alibainisha kuwa kati yake, Sh. milioni 614.6 zinatokana na makusanyo kutoka kwa wachimbaji wadogo.
"Kiasi hicho kilichokusanywa kinazidi jumla ya makusanyo ya mrabaha wa miaka mitatu iliyopita kutoka kwa wachimbaji wadogo," alisema na kueleza zaidi:
"Pia Bunge lako tukufu litapendezwa kufahamu kwamba katika mwaka 2015 tulikusanya mrabaha wa Sh. milioni 166.8, mwaka 2016 Sh. milioni 71.8 na mwaka 2017, Sh. milioni 147.1 kutoka kwa wachimbaji wadogo."
Waziri huyo pia alisema wizara inaendelea kufanya ukaguzi wa uzalishaji wa madini kwenye migodi mbalimbali kuhakikisha inapata takwimu sahihi za madini yanayozalishwa na kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Alisema ukaguzi huo hususan kwenye migodi na mitambo ya uchenjuaji, umekuwa ukifanyika kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
"Kutokana na jitihada hizo, makusanyo ya mrabaha yameongezeka. Hadi kufikia Machi mwaka huu, Ofisi ya Madini iliyopo Chunya ilikuwa imekusanya Sh. milioni 718.6 na Ofisi ya Madini Mwanza ilikuwa imekusanya Sh. bilioni 9.8 ikilinganishwa na Sh. milioni 416.9 na Sh. bilioni 6.1 zilizokusanywa na ofisi hizo kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 kwa mfuatano huo," alisema.