Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, amesema kuwa hakuna sababu ya msingi kwa mtu yeyote nchini ambaye ana hoja za kutilia shaka utendajikazi wa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli labda kuwe na sababu nyingine ambazo ni nje ya utendajikazi.
Mongella ameongea hayo Juni 17, 2018 wakati wa uzinduzi wa kivuko kipya cha MV Mwanza ambacho kitafanyakazi katika eneo la Kigongo-Busisi, na kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kufanya mambo makubwa katika kipindi cha muda mfupi tangu kuingia madarakani chini ya Rais Magufuli.
“Unaweza kumsema Magufuli labda hupendi sura yake, lakini huna namna ya kusema huyu mtu hafanyikazi, Serikali inapiga kazi leo tunaona meli MV Mwanza itaenda pale Kigongo feri kwenda Busisi ina uwezo mkubwa, ni jambo kubwa hii meli ni ya kisasa zaidi ni nyepesi, ina kwenda kasi na inabeba mzigo mkubwa” amesema Mongella
Mongella ameongeza kuwa kivuko hicho cha kisasa kitasaidia ufanisi katika sekta ya usafiri wa majini katika ziwa victoria kwasababu itasafirisha mizigo mikubwa kwa wakati mmoja na kwa gharama nafuu na kuwataka wananchi kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli.
Kivuko cha MV Mwanza kina uwezo wa kubeba uzito wa tani 250, kitafanya kazi katika eneo la Kigongo–Busisi Mkoani Mwanza na utengenezaji wake umegharimu jumla ya shilingi bilioni 8 na kitaweza kubeba abiria 1000 na magari 36 kwa wakati mmoja.