Wabunge CCM wazomeana kisa korosho

Sakata  la malipo ya mauzo ya korosho limeendelea kuteka mjadala wa Bunge, safari hii likisababisha watunga sheria kutoka chama tawala CCM kuzomeana huku Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara 'Bwege' (CUF) akitolewa ukumbini kwa kuchochea vurugu ndani humo.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Bukoba Vijijini, na Katibu wa Wabunge wa CCM, Jason Rwekiza, alisema kuwa analazimika kufafanua kauli iliyotolewa na Hawa Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kuwa kipo kikundi cha wabunge wanaotaka kuwachafua.

Alisema yeye akiwa ni Katibu wa Wabunge wa CCM ndiye anayepanga wachangiaji wa chama hicho bungeni.

"Nalisema hili kwa sababu Mheshimiwa Hawa Ghasia amesema kuna watu wamepangwa na serikali kuwachafua, hii siyo sahihi," Rweikiza alisema. "Orodha ya wachangiaji nimepanga mimi, naomba mnisikilize tulia… tulia... nisikilizeni," alisisitiza mbunge huyo baada ya kuibuka zomeazomea dhidi yake bungeni.

Katika mjadala huo, Ghasia alisema anasikitishwa na maneno yanayosambazwa kwa makusudi dhidi ya wabunge wanaotetea kupelekwa pembejeo kwenye maeneo yao.

"Kuna taarifa kuwa jana (juzi) watu walikaa vikao, wameandaliwa kuja bungeni kuwadhalilisha wabunge hao wanaotetea wananchi, ili wapate pembejeo na kutetea wakulima wapate fedha zao," Ghasia alisema na kueleza zaidi:

"Wabunge wote humu ndani tuna haki sawa za kutetea wananchi wetu. Anayetoka kwenye pamba ataitetea, anayetokea kwenye madini atatetea madini yake na korosho ana haki ya kuitetea korosho yake.

"Na mimi napenda niwahakikishie wananchi kwa ujumla kuwa wabunge wake tupo imara. Tutapambana kuhakikisha haki hii inapatikana na hata isipopatikana, wajibu wetu tutautimiza kama wawakilishi wa wananchi ambao tulichaguliwa kuja kuwatetea bungeni.

"Leo tunaambiwa kuwa eti ni wabinafsi, na ni mbinafsi? Kuna watu wanakuja kusimama wanasema wao ndiyo wanaijua korosho kushinda mtu mwingine humu ndani."

Alisema hata ukifika Chuo Kikuu cha Mzumbe, utakuta ripoti za utafiti wake kuhusu korosho na hata utafiti wake wa shahada yake ya uzamili ulikuwa unahusu namna ya kuifufua korosho na kuitafutia soko.

Kama ilivyokuwa wiki iliyopita wabunge wa pande zote mbili waliendelea kuibana serikali kulipa kiasi hicho cha fedha walipokuwa wanaendelea na mjadala wa mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017.

Hoja hiyo imeteka mjadala huo kutokana na serikali kuonekana kushindwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya Tasnia ya Korosho, inayotaka asilimia 65 ya mauzo ya korosho inatakiwa irudishwe Bodi ya Korosho na asilimia 35 inatakiwa kupelekwa Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kabla ya mjadala huo kuanza Jumatatu iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Hawa Ghasia, aliwasilisha taarifa ya kamati yake bungeni siku hiyo na kueleza kuwa serikali imeshindwa kupeleka kwenye Bodi ya Korosho Sh. bilioni 201.281.

Kati yake, Sh. bilioni 91.15 ni za mwaka 2015/16 na Sh. bilioni 110.131 ni za mwaka 2016/17.

Ghasia alibainisha kuwa serikali imepeleka Sh. bilioni 10 kwenye mfuko hivyo, bado unaidai Sh. bilioni 81.15 za msimu uliotangulia, hivyo kuathiri zao hilo kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa pembejeo.

Wakati kamati hiyo ikieleza hayo, jana Mbunge wa Mtama, Nape Nauye (CCM), alisema kuna uwezekano wa kuizika CCM mikoa ya kusini kama serikali haitatoa fedha hizo.

Alisema kuwa aliwahi kutoa hoja bungeni kuhusu suala hilo akitaka kusimamia utekelezaji wa sheria, lakini cha kushangaza anaona serikali inaacha kutekeleza sheria iliyopo huku ikiwasilisha mapendekezo bungeni kufuta ulipaji wa fedha hizo kwa wakulima na badala yake ziende serikali kuu.

Alisema kitendo hicho ni hatua ya serikali kuonyesha dharau kwa wakulima na Bunge, jambo alisisitiza si sawa na haikubaliki.

“Mimi nadhani maoni yangu hebu tuzungumzie namna ya kuleta fedha mlizochukua, hii habari ya kubadilisha sheria iacheni kwanza," Nape alisema.

"Maisha haya ni yetu, tusifike mahali tukafika huku maana ni pabaya sana. Leo mnataka kutupeleka kwenye korosho na hela mliyotarajia kuipata hamtaipata tena maana zao hilo linakufa.

“Mapendekezo yangu tuzungumzie namna ya kupata hela yetu, kueni na huruma kwetu na mapendekezo haya yanaenda kutuweka mahali pagumu sana.

“Nataka kuwaanbia, msipopeleka fedha za korosho kwa wakulima mtakuwa mmeizika CCM kabisa katika mikoa ya kusini maana kutakuwa hakuna namna nyingine ya kuweza kujinasua."

Wakati Nape akichangia, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, alisimama kutoa taarifa, akimtaka mbunge huyo kutowatia hofu wakulima wa korosho nchini.

Kutokana na hali ya zomea zomea na vurugu, Mwenyekiti wa Bunge, Azzan Zungu aliyekuwa anaongoza kikao cha jana, alisimama na kuwataka wabunge watulie, akieleza kuwa kila mtu ana uhuru wa kuchangia.

Rwekiza aliendelea kuchangia, akieleza kuwa orodha ya wachangiaji huwa anaipanga yeye na kwamba Ghasia hakupangwa licha ya kuwa kupata nafasi hiyo jana.

Wakati mjadala huo ukiendelea, Zungu alitoa angalizo la mwisho kwa wabunge waliokuwa wanapiga kelele kwa kuzomea na baadaye akaagiza Bwege atoke ndani ya Ukumbi wa Bunge kutokana na kusababisha vurugu.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad