Wabunge Watakiwa Kuwasilisha Taarifa za Mali Wanazomiliki Ili Zikaguliwe

Wabunge Watakiwa Kuwasilisha Taarifa za Mali Wanazomiliki Ili Zikaguliwe
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka wabunge wote kuwasilisha taarifa za mali wanazomiliki kwa Katibu wa Bunge kabla ya Juni 25, 2018.


Akitoa taarifa ya hiyo ya Sekretarieti leo Naibu Spika Dk Tulia Ackson amesema Sekretarieti ilitoa muda kwa wabunge kuwasilisha taarifa za umiliki wa mali zao na kwamba wabunge wengi hawakutekeleza agizo hilo.

“Sekretarieti iliwataka kuwasilisha nyaraka kabla ya Juni 25, 2018 zinazohusu fedha zilizoko benki au taasisi zingine za fedha, hisa, majengo, nyumba, madeni, mashine, viwanda, mitambo, magari na aina nyingine za usafiri, madeni na mikopo kwa mali zote zilizopo nje,” amesema.

Dk. Tulia amewafahamisha wabunge kwamba mwakilishi wa Kamishna atafika ofisini kwa Katibu wa Bunge kuchukua taarifa za wabunge.

Pamoja na taarifa hiyo Dk Tulia amesema kwa kuwa kuna kundi ambalo halikuwa na taarifa kuhusu kuwasilisha vielelezo vya mali zao wataangalia jinsi ya kuwasiliana nao ili kuona vitawasilishwa lini mara baada ya kurudi kwenye majimbo yao.

Naye Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga (CCM) ameitaka serikali kuhakikisha uhakiki wa mali za wabunge unaenda sanjari na uhakiki wa kiwango cha elimu na taaluma zao.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad