Wafikishwa Mahakamani Baada ya Kukutwa na Ngozi ya Chui

Wafikishwa Mahakamani Baada ya Kukutwa na Ngozi ya Chui
Wakazi wawili wa Mburahati Kisiwani, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kukutwa na ngozi ya chui.

Akizungumza leo Juni 18 Wakili wa Serikali, Kandidi Nasua aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Vicent Mteleka(75) na Christopher Kipilili( 51).

Wakili Nasua, amedai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Hamisi Ally, kuwa washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la uhujumu uchumi.

Nasua alidai kuwa, Mei 9, 2018 katika eneo la Mburahati Kisiwani , wilaya ya Kinondoni, washtakiwa walikutwa na ngozi ya chui yenye thamani ya Sh 8milioni bila kuwa na leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini, huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka linalowakabili,  hawakutakiwa kusema chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina  uwezo wa kusikiliza shauri hilo.



Hata hivyo, Wakili anayewatetea washtakiwa hao, Amon Ndunguru ameiomba Mahakama iwapatie dhamana wateja wake kwa sababu wamekaa mahabusu kwa muda mrefu kabla ya kufikishwa mahakamani.

“Kuzuia dhamana bila kuwa na hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ni kwenda kinyume na sheria, hivyo naiomba mahakama yako iwapatie dhamana wateja wangu”amedai Wakili Ndunguru.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Ally amesema kwa mujibu wa thamani ya nyara zilizokamatwa ni chini ya Sh 10milioni, hivyo mahakama hiyo inayo mamlaka ya kutoa dhamana.

Hakimu Ally aliyataja masharti ya dhamana kuwa ni kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika, anayetambulika kisheria atakayesaini bondi ya Sh9 milioni.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 2, mwaka huu itakapotajwa na mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad