Mgawanyiko wa dhahiri umeanza kujitokeza wazi ndani ya chama cha ANC huku wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Jacob Zuma wakipinga kuhutubiwa na mwenyekiti Gwede Mantashe aliyegemea upande wa Rais Cyril Ramaphosa.
Wafuasi wa Zuma Ijumaa usiku walizusha tafrani katika mkutano wa jimbo kwa kumzomea Mantashe alipopanda jukwaani kutaka kuzungumza.
Waliokuwa wakizomea ni wafuasi wenye hasira, ambao kwa wazi kabisa walionekana kuwa wafuasi wa Zuma walikuwa wakiimba “Wenzeni uZuma‚ wenzeni uZuma” yaani “Zuma amewakosea nini?”
Mantashe‚ aliyekwenda kwa ajili ya kutoa hotuba kwa niaba ya uongozi wa ngazi ya juu ya chama, alizuiwa kuzungumza licha ya mratibu wa jimbo hilo Shle Zikalala kujaribu kuwasihi waache kuimba.
Mwandishi wa mtandao wa SowetanLIVE alishuhudia wajumbe wengi wakiimba na kupiga meza kila Mantashe alipojaribu kuzungumza.
Hata hivyo, Mantashe alisema atazungumza vivyo hivyo licha ya kelele zilizokuwa zikitolewa na aliowaita “watu wachache”.
“Kwa bahati mbaya nitazungumza hapa usiku leo labda kama huu si kutano wa ANC. Ikiwa huu ni mkutano wa kikundi kilichoasi‚ basi sitazungumza,” alisema Mantashe. Kutokana na hali kuendelea kuwa tete waandishi wa habari waliamliwa baadaye kuondoka.
Taarifa zinasema Mantashe alizomewa yakiwa ni matokeo ya yeye kuwa upande wa rais wa ANC Cyril Ramaphosa katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Desemba mwaka jana.
Mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa jimbo hili ulitarajiwa kufanyika Ijumaa na kumalizika Jumamosi lakini ulivurugwa na wanachama wasioridhishwa na hali ilivyo.
Mahakama Kuu ya KwaZulu-Natal mjini Pietermaritzburg ilitoa amri ya kusitishwa uchaguzi. Kesi itasikilizwa Julai 7.