Waliovamia Pori la Akiba Wapewa Siku 30 Kuondoka

Waliovamia Pori la Akiba Wapewa Siku 30 Kuondoka
Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewapa siku 30 wananchi waliovamia pori la akiba Swagaswaga na kuendesha shughuli zao ikiwemo kilimo, makazi na ufugaji ndani ya pori hilo na kutakiwa waondoke kwa hiara yao kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Handa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua mgogoro wa ardhi kwenye hifadhi hiyo wilayani humo.

"Tunawapa siku 30 muanze kutoka wenyewe, baada ya siku 30 tunatoa notisi ya siku nyingine 30 za kutumia nguvu, kwahiyo kuanzia sasa hivi anzeni kujipanga wenyewe na kuondoka wakati Halmashauri ikifanya tathmini ya maeneo ya vijiji ambavyo ni halali ya kuwagawia kwa wale watakaopenda kupewa maeneo huko", amesema Dkt. Kigwangalla.

Aidha, Waziri Kigwangalla amesema sheria za uhifadhi haziruhusu mtu yeyote kuingia ndani ya maeneo ya hifadhi na kuendesha shughuli za kibinadamu na kwamba kufanya hivyo ni kudharau Sheria na Malmlaka zilizopo.

Kwa upande mwingine, Dkt. Kigwangalla amesema kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Handa ambacho kilianzishwa kimakosa ndani ya pori hilo wataendelea kubaki mpaka pale wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Tamisemi na Ardhi zitakapoamua hatma yao ikiwemo ama kulipwa fidia kupisha eneo hilo au waendelee kubaki na mipaka ya hifadhi isogezwe.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad