Uongozi wa Klabu ya Mabingwa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC umefunguka na kudai katika kuelekea usajili wa ligi Kuu msimu ujao watahakikisha wanaongeza wanaume zaidi kuliko waliokuwa nao katika kipindi hiki ambao wamewapa mafanikio makubwa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Haji Manara leo Juni 25, 2018 na kusema walichekwa na kudhalilishwa sana kwenye msimu ulioisha kwa kusajili wachezaji wazee kama watu wasemavyo lakini ndio waliowawezesha kupata ubingwa.
"Nakumbuka vema tulipowasajili hawa Wanaume (John Bocco, Emmanuel Okwi na Erasto Nyoni) jinsi tulivyodhihakiwa, waliitwa wahenga tukaambiwa tumesajili 'ICU' na maneno mengi. Tena hata baadhi ya wanasimba walitulaumu viongozi",ameandika Manara.
Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusisitiza kuwa "tulijua 'what we did' na imelipa, hao ndio wachezaji bora katika msimu huu. Hakuna ubishi na sijasikia lalamiko lolote, sasa 'for next season' pamoja na usajili tulioufanya tutaongeza wanaume. Tunayakumbuka vema maelekezo ya Mh Rais wa nchi".
Majigambo hayo ya Haji Manara yamekuja baada ya kupita siku moja tokea zilipotolewa Tuzo za Ligi Kuu Tanzania Bara na timu yake kuweza kuchukua Tuzo nyingi zaidi ya washiriki wengine waliokuwepo katika kinyang'anyiro hicho licha ya maneno mengi yaliyokuwa yanaiandama timu yake kuwa ilisajili wachezaji wazee ambao wasingeweza kuitumikia klabu ipasavyo lakini ikawa ndivyo sivyo.